November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Simbachawene aipongeza LSF kuzindua mpango mkakati mpya 2022/2026

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene (wa pili kushoto), ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 10 ya LSF, akimkabidhi tuzo Msaidizi wa Kisheria kutoka Zanzibar, Hija Masoud Ame (wa tatu kushoto), ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng'wanakilala na kulia ni Mwakilishi wa DANIDA, Mette Bech Pilgaard wakati wa pili kulia ni Mkuu wa Masuala ya Siasa wa Uingereza hapa nchini Tanzania, Laurence R Wilkes.

Spread the love

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Mpango wa Miaka mitano wa Shirika la Huduma za Msaada wa Kisheria (LSF) utasaidia upatikanaji wa haki nchini na kuweka mazingira bora kwa wanawake kuchangia katika shughuli za uchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 10 ya LSF, Waziri Simbachawene alisema Mpango mkakati huo wa mwaka 2022 hadi mwaka 2026 utatoa dira na mwelekeo wa taasisi hiyo.

Pia alisema utainisha vipaumbele vyake vitakavyoweza kusaidia upatikanaji wa haki nchini na kuweka mazingira bora kwa wanawake kupata haki zao katika kuchangia shughuli za uchumi kuboresha maisha yao na familia zao kwa ujumla.

“Naipongeza LSF kwa kuzindua mpango mkakati mpya wa miaka mitano 2022/2026, ambao umelenga kufanya kazi kwa karibu na serikali na Taasisi zake katika kuboresha sera, sheria, na kuweka mazingira bora na wezeshi kwa jamii hususani wanawake wanawake.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 10 ya LSF, akimpatia tuzo Aziza Ali Choro kutoka Zanzibar kwa kuwa kinara wa kuhamasisha upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana. Kulia ni Mwakilishi wa DANIDA, Mette Bech Pilgaard wakati wa pili kulia ni Mkuu wa Masuala ya Siasa wa Uingereza hapa nchini Tanzania, Laurence R Wilkes. Nyuma yao ni Mwenyekiti wa Bodi ya LSF Bengi Issa.

“Naipongeza Taasisi hii ya LSF, kwa tukio hili muhimu la kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011. Tukio hili hili sio tu muhimu kwa LSF, bali kwa nchi yetu hususani wadau wa ufikiaji na upatikanaji wa haki nchini kote,” alisema.

Alisema awali serikali ilikuwa ikitoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watuhumiwa walioshtakiwa kwa makosa makubwa kama vile mauaji, kuua bila kukusudia na uhaini ambapo huduma hiyo kwa muda mrefu ilikuwa ikitolewa na mahakama kuu pekee.

“Asasi mbalimbali za kiraia zilikuwa zikitoa baadhi ya huduma za kisheria kuanzisha ushauri wa kisheria na uwakilishi mahakamani, kazi hii ilikuwa ikifanywa pasipokuwa na utaratibu baina ya taasisi hizo na serikali,” alisema.

Aidha, akizungumzia mpango huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala alisema Mpango mkakati wa mwaka 2022 hadi 2026 umelenga kufanya kazi kwa karibu na serikali na taasisi mbalimbali katika kuboresha sera, sheria na kuweka mazingira bora na wezeshi kwa jamii hususani wanawake na watoto kupata huduma ya msaada wa kisheria.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 10 ya LSF akimpatia tuzo mwakilishi wa Shirika la BAKAID Mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya kutambua juhudi zake katika kujengea uwezo mashirika wanufaika wa LSF. Kulia ni Mwakilishi wa DANIDA, Mette Bech Pilgaard wakati anayeshuhudia katikati ni Mwenyekiti wa LSF, Bengi Issa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya LSF Bengi Issa alisema kwa miaka 10, LSF imekuwa ikitekeleza program mbalimbali  ya kuwasaidia wanawake kupata msaada wa kisheria.

“Watanzania wamekuwa wakipata msaada wa kisheria kwa urahisi bila kutaabika kwenda kwenye mahakama na kutumia gharama,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Malinyi (BPO), Rashid Kiding’a alisema; “Naishauri Serikali ituangalie kwa jicho la tatu sisi wasaidizi wa huduma za kisheria kwa sababu tunafanya kazi ngumu katika mazingira magumu sana.

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo Denmark- DANIDA, Mette Bech Pilgaard alisema kwa miaka 10 LSF imekuwa ikitekeleza programu kubwa ambayo inagusa wananchi wa kawaida, hali ambayo iliwafanya kuwa wawezesha wakubwa wa kipindi chote cha miaka yake 10.

Katika kipindi cha miaka 10 LSF imetoa ruzuku kwa mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 200 Tanzania Bara na Visiwani.

error: Content is protected !!