Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Maisha Afya Siku 25 zilivyopukutisha Vigogo wa Wizara ya Afya
AfyaHabari za SiasaTangulizi

Siku 25 zilivyopukutisha Vigogo wa Wizara ya Afya

Dk. Nyambura Moremi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya
Spread the love

DK. Faustine Ndigulile, amekuwa kiongozi wa sita, ndani ya wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, kuenguliwa kwenye wadhifa wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Safari ya Dk. Ndugulile kuhudumu nafasi ya naibu waziri wa afya nchini Tanzania, aliyoianza tarehe 9 Oktoba, 2017, aliihitisha juzi Jumamosi, saa 2 usiku wa tarehe 16 Mei, 2020 baada ya Rais John Magufuli kutangaza kutengua uteuzi wake.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ilisema, Rais Magufuli amemteua Dk. Godwin Mollel, Mbunge wa Siha (CCM) kuchukua nafasi ya Dk. Ndugulile.

Vigogo hao wote wa afya, wameenguliwa katikati ya vita ya mapambano ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ambao kwa nafasi zao walikuwa wahusika wakuu kwenye vita hiyo.

Itakumbukwa, mgonjwa wa kwanza wa corona alilipotiwa Tanzania tarehe 16 Machi, 2020 mkoani Arusha kisha kusambaa mikoa mbalimbali.

Takwimu za mwisho kutolewa na serikali, zilionyesha wagonjwa wamefikia 509, vifo 21.

Hata hivyo, jana Jumapili, Rais Magufuli alilieleza Taifa kwamba hali ya ugonjwa huo si mkubwa kwani wagonjwa wengine wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Siku 25 za vigogo hao kuenguliwa, zilianza tarehe 22 Aprili, 2020 kwa Dk. Zainabu Chaula kuhamishwa kutoka katibu mkuu wizara ya afya na kupelekwa katibu mkuu wa Mawasiliano akichukua nafasi ya Dk. Maria Sasabo ambaye amestaafu.

Dk. Chaula amehudumu wizara ya afya takribani mwaka mmoja na miezi mitatu kuanzia tarehe 8 Januari, 2019 akichukua nafasi ya Dk. Mpoki Ulisubsya aliyeteuliwa kuwa balozi.

Dk. Faustine Ndungulile, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya

Nafasi ya Dk. Chaula ambaye ni daktari wa magonjwa ya binadamu aliteuliwa
Profesa Mabula Daudi Mchembe.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Machembe alikuwa Msaidizi wa Rais Magufuli katika masuala ya afya.

Siku hiyo hiyo ya tarehe 22 Aprili, 2020, Rais Magufuli alimteua Profesa Abel Makubi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali kuchukua nafasi iliyoachwa na Profesa Mohamed Bakari Kambi aliyestaafu.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Makubi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza.

Panga pangua hiyo ndani ya wizara ya afya iliendelea tarehe 3 Mei, 2020 ambapo Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Laurean Rugambwa Bwanakunu, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD).

Badala yake, Rais Magufuli alimteua Brigedia Jenerali Dk. Gabriel Mhidize kuchukua nafasi ya Bwanakunu.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mhidize alikuwa Mkuu wa Hospitali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Lugalo Jijini Dar es Salaam.

Laurean Rugambwa Bwanakunu, aliyekuwa Mkurugenzi wa MSD

Bwanakunu aliongoza MSD kuanzia tarehe 23 Juni, 2015 baada ya kuteuliwa na Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Kabla ya uteuzi huo, Bwanakunu alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ariel Glaser Paediatric AIDS Healthcare Initiative.

Kuwekwa kando kwa bosi huyo wa MSD, kulifuatiwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kesho yake yaani tarehe 4 Mei, 2020 kumwagiza katibu mkuu wizara hiyo, kuwasimamisha kazi, Dk. Nyambura Moremi, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na Jacob Lusekelo, Meneja Udhibiti wa Ubora ili kupisha uchunguzi.

Pia, aliunda kamati ya wataalamu wabobezi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa maabara hiyo, ikiwemo mfumo mzima wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za Covid-19.

Kamati hiyo ya watalaamu nane wabobezi, wakiongozwa na Prof. Eligius Lyamuya, kutoka Chuo Kikuu cha Afya Shirikisho Muhimbili (MUHAS), ilitakiwa kuwasilisha kwa waziri wa afya, taarifa ya uchunguzi huo kabla ya aterehe 13 Mei 2020.

Jana Jumapili, Rais Magufuli akizungumza kanisani ushirika wa KKKT Chato, mkoani Geita alisema taarifa ya kamati hiyo imekamilika na Waziri Ummy aliyeiunda ataitoa kwa umma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Afya

Mloganzila yajipanga kupandikizaji wa ini

Spread the love  HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imesema kutokana na uwekezaji uliofanywa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!