December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kujenga Shule 1,000 za Sekondari

Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Spread the love

SERIKALI inatarajia kujenga shule mpya za Sekondari 1,000, kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), ili kuondoa changamoto ya upungufu wa madarasa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa jana tarehe 22 Desemba 2020 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako katika ziara yake aliyoifanya kwenye Shule ya Sekondari Kibaigwa, iliyoko mkoani Dodoma.

Prof. Ndalichako ametoa taarifa hiyo wakati anatoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya upungufu wa madarasa, iliyosababisha wanafunzi zaidi ya 74,000 katika mikoa 17 kuchelewa kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

“Sasa ili kutatua changamoto hii, katika mradi wetu wa kuimarisha elimu ya sekondari, tunataka kujenga shule mpya 1000. Kwa hiyo tunaamini kwamba itataua tatizo hilo,” amesema Prof. Ndalichako.

Licha ya ujenzi wa shule hizo mpya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jaffo, iliagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa unakamilika kabla ya mwezi Februari 2021, ili wanafunzi watakaochelewa kujiunga na kidato cha kwanza, waanze masomo.

Akitoa sababu ya upungufu wa madarasa, Prof. Ndalichako amesema inasababishwa na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya Sekondari kutokana na utekelezwaji wa sera ya elimu bila malipo.

“Wakati mwingine wananchi wana kuwa hawatuelewi kwamba kwa nini hatujajipanga, kwa nini madarasa yanakuwa hayapo. Ni kwa sababu ile kasi ya wanafunzi kuongezeka imekuwa kubwa mno, ni matunda ya elimu bila malipo,” amesema Prof. Ndalichako.

Hata hivyo, Prpf. Ndalichako amesema ujenzi wa madarasa katika mwisho wa mwaka husuasua kutokana na wakurugenzi wengi wa halmashauri kuwa likizo.

“Serikali imeliona hili suala na kila mwaka ikifika mwishoni tunakuwa tunakimbizana kujenga madarasa huku wakurugenzi wanakuwa wengi likizo, inakuwa kama utamaduni,” amesema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako ametolea mfano Shule ya Sekondari Kibaigwa, ambayo imepokea wanafunzi wengi ikilinganishwa na idadi ya madarasa yake.

“Mwaka huu wanaokuja kuanza kidato cha kwanza ni zaidi ya 450, lakini waliondoka mwaka uliopita ambao walikuwa kidato cha nne ni zaidi ya 236.

Kwa hiyo ni dhahiri kwamba kutakuwa na upungufu wa madarasa, kwa sababu hao walio ondoka nafasi waliyokuwa wanaitumia, itakuja kutumiwa na hao wanaokuja ambao ni karibu na mara ya mbili yake,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri huyo wa elimu ametoa ufafanuzi huo siku kadhaa baada ya kusema wanafunzi zaidi ya 74,000, watachelewa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma hivi karibuni, Jaffo alisema upungufu huo umetokea katika mikoa 17 ikiongozwa na Dar Es Salaam, Arusha na Dodoma.

error: Content is protected !!