WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja jipya la Tanzanite (Salander), lililoko jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam…(endelea).
Waziri Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja hilo leo Jumanne tarehe 22 Desemba 2020.
Akizungumza katika ukaguzi huo, Waziri Majaliwa ameiagiza Kampuni inayojenga daraja hilo, GS Engineering Corporation ya Korea Kusini, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, Waziri Majaliwa amesema ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri.

“Nimekagua mradi na ujenzi wake unaendelea vizuri, sina mashaka na viwango na naamini utakamilika kwa wakati. Watanzania wanasubiri kwa hamu waanze kupita katika daraja hili,” amesema Waziri Majaliwa.
Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Christianus Ako amesema daraja hilo maarufu kama Salander lenye urefu wa kilomita 1.03 na upana mita 20.5, ujenzi wake unatarajia kukamilika Oktoba 2021.
Mhandisi Ako amesema ujenzi wa daraja hilo unaogharimu Sh 243 bilioni, una lengo la kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambayo inatumiwa na magari mengi yanayoingia na kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa miradi TANROADS, amesema hadi kufikia tarehe 30 Novemba 2020, ujenzi wake ulifikia asilimia60.8.
Akieleza faida ya mradi huo, Mhandisi Ako amesema umeajiri wafanyakazi 590, kati yao asilimia 92 ni Watanzania na asilimia nane ni wataalamu kutoka nje ya nchi.
Mhandisi Ako amesema mradi huo unaendelea kutoa mafunzo kwa wahandisi 24 wa Kitanzania kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (5), wahandisi wahitimu (12) na wanafunzi wa uhandisi kutoka vyuo vikuu (7).
“Mafunzo haya yatawajengea uwezo na ujuzi utakaosaidia Taifa hapo baadae,” amesema Mhandisi Ako.
Imekula kwenu, mlikuwa hamjajipanga chadema! Mnakuwa kama hamjui siasa bwana!