Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli awaonya wanahabari, asema hawana uhuru
Habari za SiasaTangulizi

Rais Magufuli awaonya wanahabari, asema hawana uhuru

Harrison, Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akiwasili ofisi za Habari Maelezo muda mchache baada ya kuapishwa. Picha ndogo Rais John Magufuli.
Spread the love

RAIS John Magufuli leo amewaonya waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kwa namna wanavyofanya kazi yao. “Be careful, watch it. Sasa mnafikiri mna uhuru wa namna hiyo? not for that extent,” anaandika Pendo Omary.

“Ukisoma tu magazeti ya leo, picha yote, heading (kichwa cha habari), picha ya mtu ambaye alifanya kosa moja kana kwamba hicho kitendo kimefanywa na serikali. Page (ukurasa) ya kwanza, page ya pili. That is a story (habari ndio hiyo),” amehoji Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameyaeleza hayo ukumbini Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapisha mawaziri wawili, makatibu wakuu na mabalozi wapya aliowateua hivi karibuni.

Mawaziri walioapishwa ni Profesa Palamagamba Kabudi, anayekuwa waziri wa Katiba na Sheria, na Dk. Harrison Mwakyembe ambaye amebadilishiwa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mawaziri hao waliteuliwa mapema jana katika mabadiliko yaliyomaanisha kumuondoa Nape Nnauye kwenye wizara ya habari, ambayo alimteua wakati wa kuunda serikali mapema mwaka jana.

Nape ameondolewa siku moja baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa tukio la Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saam kuvamia kituo cha televisheni na redio cha Clouds Media. Aliahidi kuikabidhi ripoti hiyo kwa mamlaka ya juu yake, akitaja Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais.

Katika ripoti hiyo iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbas, na kujumuisha wahariri wa vyombo vya habari nchini, imethibitishwa kuwa Makonda alifanya uvamizi huo usiku Ijumaa ya 17 Machi 2017 akitumia askari wa serikali waliobeba silaha za moto.

Rais Magufuli hakutoa mifano iliyo wazi lakini alisema vyombo vya habari – na kutoa mfano wa yaliyotokea nchini Rwanda – vinaweza kusababisha vurugu, vinapoamua kutoa habari za machafuko badala ya zile za maendeleo.

Hakueleza habari za maendeleo ndio zipi; lakini aligusia alichokiita maandamano ya wakulima au wafugaji akieleza yanapendelewa kila wakati na kituo kimoja cha televisheni. Hakuitaja.

“Utakuta kwenye TV moja hivi kila wanapoandamana wakulima au wafugaji mahala fulani ndiyo heading (kichwa cha habari). Inachukua muda mrefu sana. Hiyo ndiyo stori kwao. Kila kitu chenye nia ya uchochezi fulani kwao ndiyo stori (habari).”

“Mwakyembe kafanye kazi. Nataka ufanye kazi. Kama wapo waliokuwepo hawakuchukua hatua wewe kachukue. Kwanza ni mwanasheria mzuri, umesoma mambo ya habari. Kafanye kazi serikali ipo.

“…Hatuwezi kuangamia kwa sababu ya watu wachache. Haitawezekana,” amesema Rais na kueleza halaiki iliyohudhuria hafla hiyo kwamba kurasa za mbele za baadhi ya magazeti ya leo Ijumaa, zimetawaliwa na tukio alilosema “kosa la mtu mmoja, kana kwamba hicho kitendo kimefanywa na serikali.”

Katika tukio hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Hoteli ya Protea, Oysterbay, Nape alifuatwa kwa kasi na askari asiyevalia sare na kuzuiwa kufanya mkutano alioutaka. Alipohoji “mtu” huyo ni nani, haraka huyo mtu alitoa bastola aliyokuwa ameiweka kiunoni na kumnyooshea Nape. Hapo kukatokea tafrani kwa Nape kupiga kelele kuwa kitendo hicho hakikuwa sawa.

Nape aliwasili eneo hilo akitokea jijini Arusha ambako alitarajiwa kukabidhi bendera ya taifa timu ya riadha inayokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa nchini Uganda.

Katika mkutano wake, uliotangazwa kuzuiwa na uongozi wa jeshi la polisi nchini, Nape alieleza kuwa hana kinyongo kwa kuondolewa uwaziri kwa kuwa kama ilivyokuwa alipoteuliwa, hakuulizwa na mteuzi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!