October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Kabudi atoa utaratibu wa dawa ya corona kutoka Madagascar 

Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imesema itafanyia uchunguzi dawa za kinga na kutibu ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosabaishwa na virusi vya corona (COVID-19), ilizopewa na Serikali ya Madagascar, kabla ya kuzigawa kwa wananchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi tarehe 9 Mei 2020 na Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo alikuwa anazungumzia msaada wa dawa inayodaiwa kutibu na corona iliyotolewa na nchi ya Madagascar kwa Tanzania ambayo Profesa Kabudi akiwa na wataalamu walikwenda jana Ijumaa kuichukua.

Msaada huo ulikwenda kuchukuliwa baada ya Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli tarehe 3 Mei 2020 wakati akimwapisha Dk. Mwigulu Nchembe kuwa waziri wa katiba na sheria alisema amefanya mazungumzo na Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina  ambaye amekubali kutoa msada wa dawa hizo.

Rais Magufuli alisema atatuma ndege kwenda kuchukua ahadi ambayo aliitekeleza jana Ijumaa ambapo Prof. Kabudi aliongoza ujumbe wa Serikali kwenda Madagascar kwa ndege ya serikali kuchukua msaada huo.

Katika mkutano wake leo Jumamosi na waandishi, Prof. Kabudi amesema Madagascar haikuwapa dawa iliyochanganywa, bali imewapa mitishamba iliyotumika kutengeneza dawa hizo.

Kati ya mitishamba hiyo, kuna mitishamba kwa ajili ya kutengeneza dawa za kinga na za kutibu waliokwisha kupata corona ambazo zote zitafanyiwa utafiti na wataalamu wa Tanzania ikiwamo kuzichanganya.

Prof. Kabudi amesema Madagascar imetoa dawa kwa ajili ya raia wake wanaoishi Tanzania na kuwataka walengwa kufika katika ubalozi wao kuchukua dawa hizo.

“Kwa hiyo hizi dawa hatutazigawa kwa sasa, zitafanyiwa utafiti na wataalamu wetu waliobobea kabla ya kuanza kutumika,” amesema Prof. Kabudi

Prof. Abel Makubi, Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania amesema, baada ya utafiti wa dawa hizo kukamilika, zitafanyiwa majaribio katika makundi matatu ya wagonjwa.

Amesema makundi mawili yatafanyiwa majaribio dawa zilizotoka Madagascar na kundi la mwisho litafanyiwa majaribio ya dawa zilizotengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR).

“Dawa hii tumeipokea kama msaada sio kwa ajili ya kuanza kugaiwa itumike kwa wananchi, dawa hii tumeipokea kwa ajili tufanye mambo mawili makubwa kama serikali.”

“Mmoja, kufanya utafiti ambao utatuonyesha kama hii dawa ni salama, yaani hii dawa ya kutibu iko salama na kama haina madhara kwa wnanachi wetu, “ amesema Prof. Makubi.

Dawa ya Corona kutoka nchini Madagascar

“Wenzetu wameijaribu na kuanza kuitumia, lakini sera yetu ilivyo lazima tuipime. Jambo la pili, tutafanya utafiti wa kuangalia ubora wa hii dawa kwa ajili ya kutibu au kupunguza makali ya COVID-19, hii itafanyika baada ya kuthibitisha inafaa kwa wananchi wetu,” amesema

Prof. Makubi  amesema, “Tumepanga kuwa na makundi matatu ya wagonjwa kwa hiari yao,  la kwanza, litapata tiba ya kusapoti na si kutibu ugonjwa bali kwa ajili ya kusapoti tiba, lakini kundi la pili itapewa dawa ya juu iliyotoka Madagascar.”

Amesema kundi la tatu, litakuwa la wagonjwa ambao wataendelea kutumia dawa za hospitali lakini watapewa dawa zilizotengenezwa na NIMR.

Kwa mara kwanza Tanzania iliripoti mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 katikati ya mwezi Machi mwaka huu, ambapo hadi sasa kuna idadi ya wagonjwa 509 na vifo 21, huku watu zaidi ya 170 wakipona ugonjwa huo.

error: Content is protected !!