December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

 NBC yazindua Bima ya Kilimo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, Serikali yaunga mkono

Spread the love

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Jubilee Insurance wamezindua huduma ya bima maalum ya kilimo inayolenga kuwalinda wakulima, wavuvi na wafugaji nchini dhidi ya hasara pindi wanapopata majanga mbalimbali yanayoweza kuathiri uzalishaji wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga … (endelea).

Bima hiyo ilizinduliwa mapema hii leo Wilayani Kahama mkoani Shinyanga na Mkuu wa Wilaya hiyo, Erasto Kiswaga katika hafla fupi ambayo pia ilihusisha mafunzo kuhusu umuhimu na faida za Bima hiyo kwa wadau mbalimbali wakiwemo wakulima na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kutoka mkoa huo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara kwa wateja binafsi Benki ya NBC, Elibariki Masuke alisema ujio wa huduma hiyo  ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini kupitias huduma za kibenki zinazolenga kutatua changamoto zinazogusa sekta hiyo muhimu.

“Benki ya NBC tuinatambua vema sekta ya kilimo na zaidi tunatambua mchango wa wa wakulima katika uchangiaji wa uchumi wa nchi na kwa msingi huu tumeona ni vema kuja na Bima ya mazao kwa wakulima. Bima hii ni ya kwanza  nchini na tunaamini kwa dhati kwamba kupitia bima hii wakulima watapunguza kwa kiwango kikubwa hasara zitokanazo na majanga mbalimbali yasiyotabilika yaani yale yalio nje ya uwezo wao.’’ alisema.

Alisema ujio wa huduma hiyo utawasaidia watanzania ambao asilimia 70 wanategemea shughuli ya kilimo kwa kuwapatia uhakika wa matokeo wanayoyatarajia kupitia shughuli zao za kilimo, uvuvi na ufugaji  hata pale wanapokabiliwa na majanga ya asili ikiwemo mvua ya mawe, mafuriko, ukame, upepo mkali, moto na majanga mengine ambayo yamekuwa yakiwasababishia hasara kubwa na kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bw Erasto Kiswaga alitoa wito kwa wakulima hao kutumia fursa hiyo kukata bima ili iwasaidie kuwakinga wanapokumbwa na majanga mbalimbali huku akiitaja sekta ya kilimo kuwa miongoni mwa sekta zinazokabiliwa na majanga mengi yasiyotabirika ikiwemo mafuriko, moto, wadudu na ukame ambavyo vimekuwa vikiwasababishia hasara kubwa wakulima.

“Hizi ni dalili njema kuona sasa huduma za Bima zimeanza kuwafikia wakulima ambao kimsingi ndio kundi kubwa zaidi katika shughuli za uzalishaji hapa nchini likigusa zaidi ya asilimia 70 ya watanzania. Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa vyama vya msingi mliohuduhuria uziunduzi huu vipelekea mpango huo kwenye bodi za mazao mbalimbali  ili utaratibu wa kuwalipia bima hii wakulima uanze mara moja,’’

“Kama ambavyo wananchi wamekuwa wakitaka bima nyingine ikiwemo bima za magari  ni vema pia wawe na bima kwa ajili ya mazao yao kwa kuwa kuanzia hii leo hasara kwenye kilimo imepata tiba,’’ alisema.

Hii ndio sababu nawapongeza benki ya NBC kwa kulifikia kundi hili. Kikubwa sasa nawaomba sana NBC kwa kuzingatia umuhimu wa mpango muweze kuwafikia wakulima wote ili wanufaike na huduma hii muhimu,’’ alisema.

Awali akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo, Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki hiyo Bw  Benjamini Nkaka alizitaja bima hizo kuwa ni pamoja na bima ya Mazao inayohusisha mazao yote ya chakula na biashara  pamoja na mazao ya matunda, Bima ya Mifugo inayohusisha mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi kondoo pamoja na Bima ya samaki mahususi kwa ajili ya wavuvi.

“Pamoja na Bima hizo pia tuna Bima ya Misitu inayolenga kumkinga mkulima wa miti dhidi ta majanga kama moto, milipuko na majanga mengine ya asili yanapotokea na kuleta hasara ambapo kupitia huduma hii  mkulima ataweza kupata fidia,’’ alifafanua Bw Nkaka huku akibainisha kwamba bima zote hizo zitazotolewa kwa ada ya asilimia 7 ya thamani ya zao husika.

Zaidi, akitaja baadhi ya faida zitokanazo na bima hiyo ambayo tayari imeshaanza kutolewa kwa wakulima wa mazao ya tumbaku kwenye mikoa ya Tabora, Kigoma na wilaya ya Kahama, Bw Nkaka alisema inatoa fidia kwa wakulima na wafugaji pindi wapatapo hasara zitokanazo na majanga mbalimbali na inawapa wakulima na wafugaji uhuru na amani ya kuendelea na shughuli za kilimo bila kuhofia hasara.

“Zaidi bima hii inamnufaisha mkulima na mfugaji katika kulinda kipato chake, bila kurudi nyuma hasara inapotokea na hivyo kuwa na kilimo endelevu na pia itamuwezesha mkulima na mfugaji kujifunza zaidi hatua bora za ufugaji na ukulima.’’ Alisema akiongeza kuwa  mkulima anaweza kupata bima hiyo kwa kiwango cha chini hadi kufikia Tsh 25,000 kwa hekari moja kwa mazao yote.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima hao Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika Kahama (KACU) na Mbunge wa Jimbo la Ushetu Bw Emmanuel Cherehani alisema huduma hiyo imekuja wakati muafaka katika kipindi ambacho wakulima wamejipanga kufanya mapinduzi ya kilimo kupitia kilimo cha kisasa kinachoshusisha tahadhari zote muhimu ili kuepuka hasara ambazo zimekuwa zikiwarudisha nyuma kimaendeleo.

“Ni msimu uliopita tu wakulima tulipata hasara ya dola laki mbili katika wilaya ya Kahama tu kutokana na majanga haya. Ni kutokana na hasara kama hizo ninaomba vyama vya msingi viangalie namna ya kuwalipia wakulima bima hizi kupitia mjengeko wa bei  ili wote wawe na bima badala ya kusubiri benki ndio ianze kukimbizana nao huko,’’ aliagiza.

error: Content is protected !!