MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kata ya Kaselya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Ramadhani Hamisi (30) ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni.
Kadhia hiyo ilimkuta Ijumaa iliyopita usiku katika kitongoji cha Musisi karibu na Kaselya Mabandani ikidaiwa alikutwa akiwa na mke wa Ally thumani. Anaripoti Thomasi Kiani, Singida…(endelea).
Habari zinadai kuwa Hamisi alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa Athumani kwa muda mrefu na walishakutwa mara nyingi na kuonywa na mwenye mali aache mchezo huo. Inadaiwa siku hiyo ya Ijumaa Athumani aliwakuta nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kaselya, Wazzael Maija tukio hilo lilitokea saa 4 usiku katika kitongoji cha Musisi.
Habari zinadai kuwa baada ya Athumani kuwafuma, ugomvi uliibuka na kufukuzana gizani na kupotezana njiani lakini Athumani alimvizia nyumbani na bila kujua muda Ramadhani akamshambulia.
Inadaiwa alimchoma tumboni na kitu chenye ncha kali upande wa kulia wa tumbo na utumbo kuchomoza nje na damu nyingi kuvuja na hatimaye kuanguka.
Baada ya kubaini hivyo, Athumani alienda kwa mzazi wa Ramadhani, Ally Hamisi na kumwambia akamuone mwanae anakufa.
”Mimi tayari kazi nimeimaliza nimemkuta mwanao anamchezea mke wangu” anadaiwa kumwambia mzee huyo na kuondoka.
Habari zinadai Hamisi alipotoka nje alimkuta mwanaye hajiwezi damu ikimvuja tumboni akachanganyikiwa, lakini Ramadhani akiwa bado anafahamu kidogo akamwambia baba yake, “nikifa nimeuawa na Ali, amenichoma na kisu akakimbia.”
Mzee Hamisi alipiga yowe majirani walifika na kuamua Ali na mkewe wakamatwe wawekwe chini ya ulinzi huku Ramadhani akikimbizwa Hospitali ya mkoa wa Singida kwa matibabu.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Msisi Haruna Hamisi amesema majeruhi alipelekwa usiku huohuo Hospitali ya Singida kwa gari baada ya wananchi kumsaidia huduma za kwanza kwa kumfunga nguo jeraha hilo.
Amesema waganga wa Hospitali hiyo walijitahidi kuokoa maisha yake lakini haikuwezekana kwani muda mfupi baadae alifariki dunia kwa kutokwa na damu nyingi hasa ikizingatiwa jeraha lilikuwa pabaya
Aidha, Mwenyekiti Haruna Hamisi amesema watu waliotumwa kumthibiti Athumani na Mke wake hawakuwakuta, wote walishaondoka usiku uleule na hawajulikani walikokwenda hadi sasa.
Leave a comment