September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtulia: Yawezekana sijaiva kimkakati CCM lakini sijashindwa

Maulid Mtulia

Spread the love

MAULID Mtulia, mbunge anayemaliza muda wake wa Kinondoni jijini Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekubali matokeo na kukiri yeye bado ni mchanga kwenye siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea)

Amesema yeye hajaiva kimikakati tofauti na watia nia wenzake 79 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Mtulia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 20 Julai 2020 baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni jimbo la Kinondoni.

Katika matokeo hayo, Mtulia alipata kura 11 kati ya kura 404 zilizopigwa katika mkutano huo, huku Abbas Tarimba akiongoza kwa kupata kura 171 akifuatiwa na Iddi Azan mwenye kura 77.

Katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, Mtulia alishinda akiwa Chama Cha Wananchi (CUF) lakini tarehe 2 Desemba 2017 alitangaza kujizulu nafasi hiyo na kuhamia CCM kuunga juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya Rais John Magufuli.

Akizungumzia matokeo hayo, Mtulia amesema, “mimi bado ni mchanga kwenye siasa za chama cha mapinduzi ndio kwanza nina miaka miwili, yawezekana sijaiva kimikakati kama wenzangu walivyoiva.”

Aidha Mtulia amesema zoezi la kupiga kura lilienda vizuri na hakuna mtu mwenye manung’uniko ila kwa sasa wanakiachia chama kiendelee na mchakato wake.

“Huu ni mchakato na usiseme nimeshindwa, hizi ni kura za maoni na mchakato wa ndani ya chama bado unaendelea, kwa hiyo swala la kupata au kukosa nafasi sio wakati wake hivi sasa, tuaachia vikao vinaendelea na mchakato wa kumnpata mgombea wetu wa chama cha mapinduzi” amesema Mtulia.

error: Content is protected !!