Tuesday , 21 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mtuhumiwa ufisadi atinga TAKUKURU na gari la Jeshi
Habari MchanganyikoTangulizi

Mtuhumiwa ufisadi atinga TAKUKURU na gari la Jeshi

Spread the love

MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi, ametinga ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akitumia gari lenye namba zinazofanana na zinazotumiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kakoko alifika kwenye ofisi za makao makuu ya TAKUKURU, zilizoko Upanga, Dar es Salaam, tarehe 22 Agosti, 2022, saa mbili asubuhi, akiwa na gari hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Alikwenda kuripoti, kama alivyoelekezwa na Taasisi hiyo, wakati huu ambao uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili ukiendelea.

Bosi huyo wa zamani aliyesimamishwa kazi na Rais Samia Suluhu Hassan, mwanzoni mwa mwaka jana na kuchunguzwa na TAKUKURU, alionekana akipanda gari hilo, nje ya majengo ya ofisi hizo.

“Huyu bwana (Kakoko), alitakiwa kuripoti TAKUKURU leo, baada ya kujulishwa kuwa anatakiwa kufika mapema asubuhi. Lakini katika hali isiyotarajiwa, alifika akiwa kwenye gari la Jeshi la Wananchi,” kilieleza chanzo cha gazeti hili.

MwanaHalisi Online ilipata namba za gari hilo, lakini limeamua kuzihifadhi kwa sasa.

Aidha, MwanaHalisi Online haikufahamu mara moja gari hilo linatumiwa na ofisa gani wa Jeshi, wala Kakoko aliwezaje kulitumia na uhusiano wake na aliyekabidhiwa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za ndani ya TAKUKURU, Kakoko alitakiwa kufika hapo mapema juzi asubuhi, ili kufikishwa mahakamani.

“Lakini kile ambacho kimetushitua baadhi yetu, ni kuona anaishia kusaini na kuruhusiwa kuondoka. Tuliambiwa tayari upelelezi umekamilika na alipaswa kupelekwa mahakamani,” alieleza mmoja wa maofisa wa TAKUKURU ambaye hakupenda kutajwa.

Alisema, mtuhumiwa huyo hakuelezwa lini anatakiwa kuripoti tena TAKUKURU, badala yake aliambiwa “akihitajika atafahamishwa.”

Kakoko aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa TPA, Juni 25, 2016 na Rais John Magufuli, na amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa karibu na kiongozi huyo.

Alichukua nafasi ya Ephraim Mgawe ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Kakoko alikuwa Meneja wa Miradi katika Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Tangu kuingia madarakani Machi mwaka jana, Rais Samia amekuwa akinukuliwa mara kadhaa, kwamba baadhi ya watendaji wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wamekuwa wakihaha kutaka kumwangushia yeye ‘jumba bovu’.

Alisema: “Kuna makundi wanajua wanayofanya ndani ya Serikali. Ni makundi hayo hayo, yamekuwa yakidai kuwa ufisadi umerudi upya ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita. Mambo yako hovyo, kumbe wao ndio wako hovyo.”

Akizungumza kwa uchungu, Rais Samia alikana katakata kuwa mambo yanayodaiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali serikalini, yametendeka wakati wa uongozi wake akiwa Rais.

Alisema: “Mambo haya hayakufanyika ndani ya Awamu ya Sita, yalifanyika huko nyuma. Lakini gari bovu linaangushiwa Awamu ya Sita, sitakubali! Niliapa kusimamia haki za wananchi, nitasimama nao. Sitakubali,” alisisitiza.

Rais hajataja watendaji hao kwa majina, ingawa baadhi ya wanaosikika kutoa tuhuma hizo, walikuwa viongozi waandamizi na maofisa wa ngazi ya juu katika Serikali ya Magufuli.

Aliutaja moja ya ufisadi uliofanyika katika kipindi hicho, kuwa ni pamoja na ujenzi wa matangi ya kuhifadhia mafuta bandarini; mradi huo wa mamilioni ya shilingi aliutilia shaka na hivyo, kuagiza kusimamishwa kutekelezwa.

Aliongeza: “Naagiza TAKUKURU nendeni, pitieni fedha zote zilizokwenda kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo tunataka kuziona. Fanyeni kazi yenu, bila kuonea mtu, lakini pia bila kuogopa yeyote.”

Alipotafutwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Hamduni, ili kueleza uchunguzi wa Kakoko umefikia wapi na lini anatarajiwa kufikishwa mahakamani, alisema yuko kwenye majukumu mengine na kuelekeza kutafutwa baadaye. Hakupatikana tena hadi gazeti linakwenda mitamboni.

Lakini kumbukumbu zinaoenesha kuwa Hamduni, aliwahi kunukuliwa akisema, jalada la mtuhumiwa huyo, limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kwa hatua zaidi.

Alisema: “Suala la Kakoko uchunguzi umekamilika na tumeshawalisha taarifa ya uchunguzi wetu kwa DPP, ili kuendelea na hatua zingine za kisheria, kama ataona inafaa kwa sasa, hayo ni mamlaka yake kikatiba na kisheria. Hapo ndipo mwisho wetu, hivyo sijui ni lini atapelekwa na siwezi kumpangia.”

Alisema uchunguzi wa sakata la Kakoko ulikuwa mzito, lakini walipata ushirikiano wa kutosha kutoka taasisi zingine na hivyo, hatua zingine zinazofuata, zingefanyika muda si mrefu.

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sylvester Mwakitalu hakupatikana.

Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda alipoulizwa kuhusu gari hilo kutumiwa na raia anayetuhumiwa kwa jinai, na kama kitendo hicho hakilengi kutisha vyombo vya uchunguzi, alisema hana taarifa na kwamba yuko njiani anaendesha.

Hata hivyo, ofisa mwandamizi wa Jeshi ambaye hakutaka kutajwa jina, alipoulizwa maoni yake kuhusu sakata hilo, alisema Jeshi kama taasisi haliwezi kufanya ujinga huo, “pengine kuna mtu aliyeamua kwa sababu au maslahi yake kufanya hivyo”.

Alitaka atumiwe picha za gari hilo ili awe katika nagfasi ya kulitokea kauli, lakini aliporudiwa ili kutoa kauli simu yake iliita bila kupokewa. Na hadi tunakwenda mitamboni hali iliendelea kuwa hivyo hivyo.

Kiongozi mwandamizi Serikali aliliambia gazeti hili, kuwa kitendo cha Kakoko kutumia gari la Jeshi, kipindi ambacho bado anachunguzwa na huku amekwenda kuripoti TAKUKURU, hakioneshi picha nzuri kwa Serikali.

Alisema: “Kakoko ni mtuhumiwa wa makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Ni kiungo muhimu katika tuhuma zinazowakabili yeye na wenzake.

“Kutumia rasilimali za Jeshi, katika kipindi hiki ambacho sakata lake halijafika mwisho, ni ishara ya vitisho kwa vyombo vya uchunguzi.”

Aliongeza: “Wengine wanaweza kuona, kwamba watu wa Magufuli, bado wana nguvu na wanaendelea kumpambania, ili aonekane na vyombo vya Dola viendelee kumtambua na kumtii.”

Rais Samia aliibua ufisadi mwingine aliodai umefanyika, wakati wa uongozi ya awamu ya tano, ikiwamo utekelezaji wa miradi ambayo haikupangwa, na hivyo kufanya malipo nje ya bajeti ya Serikali.

Baadhi ya makandarasi waliotoa huduma bandarini walicheleweshewa malipo yao, hali inayosababisha madeni kuwa makubwa, kutokana na riba na hivyo, kuiongeza mzigo Serikali.

Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilifanya ukaguzi maalumu TPA, kwa agizo la Rais la Machi 28 mwaka jana, akipokea taarifa yake kwa mwaka 2019/20.

Kakoko amekuwa Mtendaji Mkuu wa TPA, katika kipindi chote cha utawala wa Magufuli. Alikamatwa Morogoro akitoka Dodoma, na baadaye alihojiwa na kuachwa kwa dhamana.

TAKUKURU imekuwa katika uchunguzi wa suala lake, tangu Juni mwaka jana, baada ya CAG kutoa ripoti yake Machi mwaka huu, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake na wenzake.

Miongoni mwa maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi, ni mfumo wa Interprise Resource Planning (IRP), ambayo ripoti yake, ilitolewa na CAG, Machi mwaka jana.

Ndani ya ripoti hiyo, kunaonekana mamilioni ya fedha yamefujwa kwa kuajiri kampuni za kuanzisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato, lakini fedha hizo hazikutoa tija kusudiwa.

Kasoro nyingine, ni baadhi ya makandarasi waliotoa huduma kucheleweshewa malipo, jambo lililosababisha madeni ya makandarasi kuwa makubwa, kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa Serikali.

Kabla ya kusimamishwa kazi na Rais, ripoti ya CAG ilibaini upungufu kadhaa, yakiwamo malipo mara mbili kwa kazi moja, au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika.

Akitoa maelekezo hayo, Rais alisema: “Kuna haja ya kufanyika ukaguzi wa kina, ili kubaini uhalali wa malipo ya fedha za Serikali kuanzia Januari mwaka huu (2021) hadi Machi.”

Rais alifikia hatua hiyo, baada ya kuelezwa na ofisi ya CAG, kwamba hali ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ni mbaya na hivyo, kunahitajika kuchukuliwa hatua za haraka.

Mbali na kuagiza kufanyika uchunguzi dhidi ya Kakoko, Rais Samia aliamuru kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi TPA, iliyofanya kazi wakati wa Kakoko, ambayo “kwa vyovyote vile, hawezi kukwepa mzigo huo.”

Akaagiza kusimamishwa ukarabati wa tagi uliokuwa unagharimu Sh bilioni 6.6 kwa tagi moja na badala yake kufanyia ukarabati kwa Sh bilioni 1.6 Kenya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Hukumu mahakama kuu yabatilishwa kesi State Oil, Equity Bank Tz

Spread the loveMAHAKAMA ya Rufani, jijini Dar es Salaam, imebatilisha hukumu iliyotolewa...

AfyaKimataifaTangulizi

Waliowekewa damu yenye VVU, homa ya ini kulipwa fidia trilioni 32.9

Spread the loveWaziri mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak ameahidi kulipa fidia ya...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali yanawa mikono fidia Kimara-Kibamba

Spread the loveSERIKALI imewataka waathiriwa wa bomoabomoa ya upanuzi wa barabara ya...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Geita, Mwanza waongoza kwa mbwa

Spread the loveNaibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema taarifa...

error: Content is protected !!