May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mtoto wa Magufuli: Mama anaumwa, anawashukuru Watanzania

Spread the love

 

JOSEPH, Mtoto wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli, amewashukuru Watanzania akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano walioutoa wakati wa kifo cha baba yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia, amesema, mama yake, Janeth Magufuli, baada ya kifo cha mme wake, John Pombe Joseph Magufuli, alipata mshtuko wa kiafya, anaendelea vizuri na matibabu huku akitoa shukrani kwa umoja waliouonyesha wakati wa msiba hadi maziko.

Hayati Magufuli, alifikwa na mauti saa 12 jioni ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam na mwili wake, kuangwa Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Chato mkoani Geita ulikozikwa 26 Machi 2021, nyumbani kwao.

Janeth Magufuli MO

Leo Jumapili, tarehe 18 Aprili 2021, kumefanyika kongamano la viongozi wa dini kuliombea Taifa na kumshukuru Mungu kwa maisha ya Hayati Magufuli.

Pia, kongamano hilo limewaombea Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Hussen Mwinyi ambaop walikuwepo kwenye kongamano hilo, lililofanyikia ukumbi wa Chimwaga, mkoani Dodoma.

Joseph, akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Magufuli, amemshukuru Rais Samia “kwa kuwa nasi katika kipindi chote ambacho tulimpoteza baba yetu, Rais wetu, mpendwa wetu.”

Pia, amewashukuru viongozi wa dini na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wote “waliokuwa pamoja kwa kumpoteza baba yetu, hadi kumfikisha kwenye nyumba yake ya milele Chato.”

Joseph amesema “nimekuja hapa kama mwakilishi, mama yangu (Janeth) hakuweza kuja, kwa sababu ya tatizo kidogo la kiafya, alipata mshtuko baada ya baba kufariki, yupo anaendelea na matibabu, anaendelea vizuri, anawashukuru sana Watanzania kwa ushirikioano waliouonyesha wakati wote wa msiba.”

“Ni suala zito la kumpoteza mzazi, mama anawashukuru sana kwa kuwa wamoja, baada ya kumpoteza aliyekluwa Rais wa awamu ya tano. Tunawashukuru na tuzidi kuliombea taifa liwe la Amani, umoja, upendo na tumtangulize Mungu kwani Mungu hashindwi kwa chochote,” amesema Joseph

Hadi mauti yanamfika, Hayati Magufuli, ameacha Mjane, Janeth na watoto saba ambao ni; Joseph, Suzana, Edna, Mbalu, Jesca, Yuden na Jeremia.

error: Content is protected !!