May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mchengerwa atangaza neema kwa watumishi

Spread the love

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, ameitaka Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ya ofisi yake, kuwatafutia watumishi wa umma na viongozi nafasi za mafunzo ya kuongeza maarifa na utaalamu ndani na nje ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mchengerwa ametoa maelekezo hayo, hivi karibuni, alipoitembelea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu yenye jukumu la kuandaa sera, miongozo na mifumo ya Usimamizi wa maendeleo ya rasilimaliwatu katika taasisi za umma ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema, Serikali inayoongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwapatia mafunzo ya kutosha watumishi wa umma na viongozi katika taasisi za umma ikiwa ni pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya, walimu au madaktari ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mchengerwa, amesisitiza kuwa Ofisi yake kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu itahakikisha Watumishi wa Umma nchini wanapata mafunzo yatakayowajengea morali na hali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ameitaka idara hiyo, kuongeza jitihada za kutafuta taasisi za kitaifa na kimataifa ambazo ziko tayari kutoa ufadhili wa mafunzo kwa watumishi na viongozi wa taasisi za umma na kuwasilisha fursa zilizopatikana kwa Katibu Mkuu-Utumishi ili aone namna bora ya kuzitoa kwa walengwa kwa kuzingatia mahitaji ya utumishi wa umma na vipaumbele vya Serikali.

Aidha, amewataka Watumishi na viongozi watakaopata fursa ya mafunzo kuwajengea uwezo watumishi na viongozi wengine ambao hawajabahatika kupata fursa ya mafunzo ili nao waweze kuboresha utendaji kazi wao.

Akipokea maelekezo ya Mchengerwa, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Elisante Mbwilo amesema, idara yake itaendelea kutafuta fursa za mafunzo kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili watumishi na viongozi wanufaike na fursa zitakazopatikana kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatekeleza jukumu la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 Kifungu G.1 (Kifungu kidogo cha 7, 9, 10 &11), Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 Kifungu cha 4.8 na Sera ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013.

error: Content is protected !!