Sunday , 28 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Mke wa Afande adaiwa kutumia nafasi ya mumewe kukomoa wenzake
Habari Mchanganyiko

Mke wa Afande adaiwa kutumia nafasi ya mumewe kukomoa wenzake

RPC Kilimanjaro, Simon Maigwa
Spread the love

JESHI la Polisi wilayani Same, linapitia wakati mgumu baada ya kilichoelezwa kuwa ni mke wa askari ambaye ni raia kutumia vibaya madaraka ya mumewe. Anaripoti Gift Mongi, Same… (endelea).

Mke huyo anadaiwa kuwasweka ndani watu anaopishana nao kauli huku akiwachangisha fedha kuwatoa.

Watu waliokumbwa na kadhia hiyo, wengi wakiwa wanawake wameiambia Raia Mwema kuwa mke huyo amekwenda mbali zaidi na kufanya wananchi waishio jirani na kambi ya Polisi, sawa na mashine ya kutolea fedha (ATM) ili wasikumbane na mkono wa sheria na kutakiwa kulipa marejesho kwa fedha wasizokopa.

Wanadai kuwa mke huyo wa askari anayejulikana kwa jina la Sara Damian amekuwa akiwatishia amani na wakilalamika, haichukui muda mara hukamatwa na kuwekwa rumande, na ili watoke, hutakiwa kutoa fedha kuanzia Sh 20,000.

Sara ambaye pia hutambulika kwa jina la Sara Salum Kabwe anadaiwa kuwatendea unyama huo, watu wanaolalamika kuwa huenda maisha yao kwa sasa yako rehani na lolote linaweza kuwatokea.

Hellen Hoseah anayeishi nje ya kambi ya kambi hiyo, ni miongoni mwa waliokumbwa na kadhia ya kuswekwa ndani na ‘Mama Afande’.

“Naomba Waziri alijue hili, lakini hata Rais Samia Suluhu Hassan ajue vijana wake wanachotufanyia, maana ni uonevu uliopitiliza sasa na anadai yeye ni sehemu ya Mamlaka, hawezi kufanywa lolote,” alilalamika Hellen kwa huzuni.

Alisema mwanamama huyo “ukibishana naye kidogo unaswekwa rumande na lawama hizo zimefika mbali zaidi kutokana na nyanyaso na kuwa ni kama Polisi inakubaliana naye.

“Alikuja nyumbani akaleta vurugu na hatimaye nikaswekwa ndani, ila hii ni hatari zaidi maana hawezi kuwa juu ya sheria, mtaa mzima tuko shakani, kwa sasa Mama (Samia) tufanyeje ujue huu uonevu?” Alisema kwa masikitiko.

“Hata Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) anayajua haya yote na alishamkanya huyu mwanamume mbele yetu, lakini bado mambo ndiyo hivi kama unavyoona, hatuna amani,” alilalamika.

Alisema anakoishi ni mtaa wa Myombo nje ya kambi ya Polisi Same, lakini ‘Mama Afande’ alimfuata na kumletea vurugu nyumbani kwake na kilichoendelea zaidi, alisombwa na polisi bila kujua shida ni nini, na ili atoke alitoa Sh 30,000.

“Yaani naishi kwa mashaka, maana sijui anajipanga kwa lipi na nikipata nafasi ya kumwona Rais, nitasema haya hapa,” alisema Hellen anayeishi nyumba namba 4 Myombo.

Esther Godfrey naye alikumbwa na kadhia ya ‘Mama Afande’, na sasa ameamua kuishi nje ya kambi, licha ya kuwa ndoa yake iko rehani na hana mustakabali mwema wa maisha yake.

Kwa sasa Esther baada ya kukimbia kwenye kambi anaishi mitaa ya Ngusero na ndoa yake iko hoi kutokana na visa vya ‘Mama Afande’ licha ya kuwa ni sehemu ya familia hiyo kwani ni wifi yake.

“Nimeamua kumwacha alivyo na aendelee tu maana yana mwisho ila sitaki kusema tena, atajua yeye mwenyewe,” alieleza Esther kwa njia ya simu akiwa kwenye makazi mapya.

“Esther ni mke wa askari pia, lakini ameachika kwa sababu ya Sara, maana alikuwa anamtumia ujumbe mume wake, ila amini tunapitia kwenye tanuru la moto,” kilidokeza chanzo kutoka kambi hiyo.

Inginahed Fanuel anatajwa pia kukumbana na sekeseke la ‘Mama Afande’ na kwa sasa ni mwaka hawasemezani licha ya kuwa na udugu.

“Nakwambia hawawezi kuongea na mbaya zaidi ni mawifi ingekuwa huku nje sawa, lakini hata familia yaani ni tatizo kubwa hapa kambini,” anaeleza msiri wa habari hii.

Sara alipoulizwa juu ya tuhuma zinazomkabili, alidai kuwa hana hadhi ya kuongea na vyombo vya habari na si kitu kipya kwake na huenda kuna wanaomwonea wivu kwa maisha yake.

“Tunaishi maisha fulani mazuri, hivyo watu wanatuchukulia poa, ila nikwambie kaka, sina muda wa kuongea na vyombo vya habari mniache,” alijinasibu ‘Mama Afande’.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Myombo, Maryciana Kagingili alipoulizwa juu ya kuswapo hali hiyo, alionekana kama kushikwa kigugumizi akishindwa kukubali au kukanusha.

“Wewe umesikia wapi? Unauliza kama nani? Naomba uniache kaka tafadhali,” alijibu Maryciana kwa njia ya simu ya mkononi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo aliiambia Raia Mwema kuwa hajapata malalamiko hayo na kama wapo walioonewa, wamfikishie taarifa ofisini mwake

“Kama kweli wapo wanaodhani wameonewa, waje ofisini watoe taarifa ila hadi sasa sijapata malalamiko yoyote,” alieleza DC Mpogolo kwa njia ya simu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipoulizwa juu ya hali hiyo, hakukubali wala kukataa, akidai atalifuatilia ili kubaini ukweli wake.

“Nadhani hao walioonewa wangefungua jalada la malalamiko, ili sisi tujue pa kuanzia, hizi ni habari mpya, nasikia kutoka kwako ila ngoja tuone,” alisema Kamanda Maigwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wami Ruvu hawana deni la Rais Samia katika kutunza vyanzo vya maji

Spread the love  BODI ya Maji Bonde la Wami Ruvu, imeendelea kuchua...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

Habari Mchanganyiko

Dk. Jafo aipongeza Oryx kumuunga mkono Samia

Spread the loveWAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na...

Habari Mchanganyiko

Mvungi aendesha kikao kazi cha wataalam wa Regrow

Spread the love  MKURUGENZI wa Idara Sera na Mipango Wizara ya Maliasili...

error: Content is protected !!