Spread the love

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema wanaanda mjadala wa kitaifa kwa ajili ya kupata maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu sifa na vigezo anavyopaswa kuwa navyo mwandishi wa habari, ikiwemo vya kitaaluma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Balile ametoa taarifa hiyo leo Alhamisi, tarehe 2 Mei 2022, akizungumza katika mafunzo ya sheria za habari Tanzani kwa wanahabari, yaliyofanyika mtandaoni.

Mwenyekiti huyo wa TEF, alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo yenye lengo la kuwawezesha wanahabari kuandika habari zinazohusu sheria za habari na mchakato wa marekebisho yake yanayoendelea sasa hivi, kuhoji vigezo sahihi vya mwandishi wa habari.

“Hilo swali limekuwa likiulizwa na watu mbalimbali, tumeona tuandae mjadala ambao uko wazi wa kitaifa ili kila mtu achangie kisha tukitoka tuwe tumekubaliana kama tunahitaji mtu mwenye sifa au mtu anayejua kusoma na kuandika awe mwanahabari au awe mtu aliyesomea taaluma,” amesema Balile.

Balile amesema, kwa sasa kuna mvutano kuhusu suala hilo, ambapo wako baadhi ya wadau wanapendekeza mwandishi wa habari awe mtu mwenye kipaji pasina kuisomea taaluma hiyo, wakati wengine wakikataa wakitaka mwanahabari awe ni mtu aliyesoma.

Katika hatua nyingine, Balile ameishauri Serikali, ifanye marekebisho katika kifungu cha tatu cha Sheria ya Huduma ya Habari ya 2016, ili kuondoa takwa lkinalomtambua mwandishi wa habari kuwa ni mtu mwenye taaluma na aliyepata leseni kutoka katika mamlaka husika.

Amesema, takwa hilo linazuia watu wa kawaida kufanya uandishi wa habari wa kijamii.

Hali kadhalika, Balile amesema TEF linaishauri Serikali ifanye marekebisho katika sheria hiyo, yatakayowezesha kila chombo cha habari kuwa na asilimia 30 ya waajiriwa wanawake, ili kupunguza changamoto ya uhaba wa wanahabari wanawake wanaoajiriwa katika tasnia ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *