Tuesday , 21 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mawakili kumtetea bure kigogo TRC, aliyetimuliwa kazi
Habari MchanganyikoTangulizi

Mawakili kumtetea bure kigogo TRC, aliyetimuliwa kazi

Spread the love

MAWAKILI kadhaa wamejitokeza kumtetea kisheria aliyekuwa Meneja wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kanda ya Dar es Salaam, Jonas Afumwisye iwapo atahitaji msaada wao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mapambano hayo yanaongozwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Peter Kibatala na wengine wengi.

Mawakili hao wanajitokeza kumtetea Jonas ikiwa imepita siku moja baada ya barua iliyoandikwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa kusambaa mitandaoni.

Katika barua hiyo yenye kurasa tatu pamoja na mambo mengine Jonas anatuhumiwa kwa utovu wa nidhamu kutokana na kuandika kwenye makundi ya kijamii ujumbe wa kupinga tozo na chanjo ya Uviko-19.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba DG/749112/180, inadaiwa kitendo hicho cha Afumwisye kukosoa uamuzi wa Serikali kinakwenda kinyume na kanuni ya 42 jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha 2 cha kanuni za utumishi wa umma ya mwaka 2003.

Akizungumza na Mwandishi Wetu juzi, Afumwisye alikiri kupokea barua ya kufukuzwa kazi kutoka TRC na anatafakari kukata rufaa kupinga uamuzi huo, kwa kuwa hakutendewa haki.

“Hiyo barua ni yangu nimepewa leo (juzi), natuliza akili ili nijue nafanyaje kama ni kukata rufaa, mimi nilisimamishwa kazi tangu Novemba mwaka jana,” alisema Afumwisye.

Alipoulizwa kama ni kweli aliandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akipinga tozo, alikana akisema si kweli, ila kwa sasa anaangalia namna ya kumaliza sakata hilo.

Hata hivyo, hakutaka kuzungumzia sakata hilo kwa undani, lakini alisisitiza kuwa hakuandika ujumbe unaodaiwa kupinga tozo, kudharau viongozi wa nchi na alishitushwa na uamuzi huo.

Akizungumzia sakata hilo Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Anna Henga alisema kituo kimesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na TRC kumfukuza, kwani iwapo alihoji jambo lolote ni haki yake kikatiba.

“Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania inatoa uhuru wa kutoa maoni kwa mwananchi yoyote wa Tanzania, ila asivunje sheria za nchi, hivyo Afumwisye ametoa maoni yake kuhusu tozo na chanjo, sisi hatuwezi kunyamaza katika hili,” alisema.

Alisema wamekuwa wakishiriki kesi nyingi za kutetea watumishi na wananchi wanaoonewa kazini, hivyo hata hili la Afumwisye iwapo atahitaji msaada, wao watamsaidia.

Anna alisema sheria na kanuni zilizotumika kumfukuza zilitumika vibaya, hivyo kuitaka Mamlaka husika kutafakari upya katika uamuzi huo.

Alisema iwapo Afumwisye alitoa kauli hizo zilizotumika kama ushahidi wa kumfukuza, anapaswa kupongezwa kwani ameonesha hisia zake kwa lile analoamini.

Anna alisema hoja kuwa Afumwisye ameshusha hadhi ya Serikali haina mashiko, kwani kiuhalisia aliyeshusha hadhi ya Serikali ni aliyeleta tozo ambazo zinalalamikiwa na wananchi.

Mkurugenzi huyo alisema suala la kutoa maoni linahusisha watu wengi, hivyo kitendo cha watumishi wa umma kubanwa katika utoaji wa maoni na Katiba ni moja si haki.

Wakili Kibatala alituma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akitangaza kwa yeyote anayemfahamu Afumwisye amjulishe awasiliane naye ili aweze kumpa msaada wa kisheria.

“Peter amejitolea kufungua kesi mahakamani, ili kutetea haki yake ya uhuru wa maoni na ajira yake bure kabisa,” alisema.

Barua hiyo ilitaja makosa hayo kuwa mosi, ni kutenda vitendo vinavyoshusha hadhi na heshima ya Serikali kinyume na kanuni ya 42 jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha 2 cha kanuni za utumishi wa umma ya mwaka 2003.

Ilidai, kwamba kati ya Julai 10 mwaka jana hadi Septemba 25 mwaka jana, Afumwisye alichangia kupitia makundi ya kijamii akitoa maneno ya kukashifu viongozi wakuu wa nchi, akiwamo Rais na Spika.

Kwa mujibu wa barua hiyo, mashitaka ya pili ni kudharau maelekezo halali ya viongozi wa kitaifa, kinyume na kanuni ya 42, jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha 3 cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.

Kwamba kati ya Julai 10 hadi Septemba 25 mwaka jana, kupitia makundi ya kijamii, Afumwisye alichangia akimtuhumu Rais kuwa anatumiwa na mabeberu na pia kuonesha vitendo vya kupinga maelekezo ya Serikali, kuhusu tozo za miamala ya simu.

Kwa mujibu wa barua hiyo, mashitaka ya tatu ni kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, akiwa mtumishi wa umma kinyume na kanuni ya 42, jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha nane cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.

Kwamba katika mashitaka hayo, barua hiyo inaeleza kuwa kati ya Julai 10 na Septemba 25 mwaka jana, Afumwisye alishindwa kuheshimu na kutekeleza kanuni za maadili na mwenendo wa kazi, kwa kuwasemea viongozi wakuu wa nchi kwenye mitandao na kupinga maelekezo ya Rais ya kukusanya mapato.

Mashitaka ya nne, ni kutenda matendo kinyume na maslahi ya umma na kanuni ya 42 jedwali la kwanza, Sehemu A kipengele cha 10 cha kanuni za umma za mwaka 2003.

Kwamba kati ya Julai 10 na Septemba 25 mwaka jana, kupitia makundi ya kijamii, alionesha kupinga juhudi za Serikali za kuainisha tozo kwenye miamala ya simu na za kuwapatia chanjo wananchi kuepuka milipuko ya magonjwa.

Kwenye mashitaka ya tano, Afumwisye anadaiwa kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma, mwenendo wa kazi na kukiuka maadili ya viongozi kinyume na kanuni ya 42 jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha 14 cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.

Kwamba ilidaiwa kuwa kati ya Julai 10 na Septemba 25 mwaka jana, kupitia makundi ya kijamii, alichangia kumtuhumu Rais kuwa anatumiwa na mabeberu na kwamba hamwamini.

Pia barua hiyo ilidai kuwa Afumwisye alitumia lugha isiyo na staha dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Baada ya kuainisha makosa hayo, barua hiyo ilihitimisha kwa kutoa adhabu ya kumfukuza kazi Afumwisye.

“Napenda kukutaarifu, kuwa baada ya uchunguzi wa tuhuma hizo kufanyika, tuhuma zote zimethibitika.

“Kutokana na tuhuma kuthibitika, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 13 (f) cha Sheria ya Reli Namba 10/2017 imeamua ufukuzwe kazi kuanzia Agosti 19 mwaka huu, kwa mujibu wa kanuni ya 42 jedwali la kwanza sehemu A, vipengele vya 2,3,8,10,14 vya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo iliendelea kueleza kuwa endapo Afumwisye hataridhika na uamuzi huo, ana haki ya kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma, ndani ya siku 45 kuanzia tarehe ya kupokea barua hiyo.

Hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 60 ya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.

Barua hiyo iliandikwa na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Kadogosa na nakala kupewa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRC.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Geita, Mwanza waongoza kwa mbwa

Spread the loveNaibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema taarifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Watumishi 25,039, taasisi 65 wahamia Dodoma

Spread the loveSerikali imesema hadi sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yapata idhini kuwa wakala wa madalali wa DSE

Spread the loveBenki ya NMB imepata idhini kutoka Benki Kuu ya Tanzania...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Waziri aipongeza NBS kwa mafanikio

Spread the loveNaibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande amepongeza Ofisi ya Taifa...

error: Content is protected !!