January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mauaji wivu wa mapenzi yatisha wanaharakati “ni janga la kitaifa”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayoshughulika na masuala ya ndoa, familia na malezi Tanzania (TaMCare), Dk. Enock Mlyuka

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeombwa itangaze matukio ya ukatili katika ndoa hasa mauaji yanayosababishwa na wivu wa mapenzi, kuwa ni janga la kitaifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo  Jumamosi, tarehe 7 Agosti 2021, katika warsha ya kuwajengea uwezo watetezi wa haki za binadamu katika kukabiliana na maafa na majanga, mkoani Dar es Salaam, iliyoandaliwa na Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayoshughulika na masuala ya ndoa, familia na malezi Tanzania (TaMCare), Dk. Enock Mlyuka, amesema matukio ya ukatili katika ndoa yanashamiri kwa kuwa hayazungumziwi kitaifa.

“Janga la ndoa na mahusiano hayazungumziwi, ikiwemo kuvunjika kwa ndoa na mauaji ya wivu wa mapenzi. Ili kukabiliana na hilo, inabidi ukatili wa kijinsia katika ndoa utangazwe ni janga la kitaifa,” amesema Dk. Mlyuka.

Dk. Mlyuka ameiomba Serikali na asasi za kiraia, ziendelee kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za matukio hayo, ili yakomeshwe.

“Msisitizo wangu ni kwamba, elimu na mafunzo kwa vijana wa kike na wa kiume wanaotarajia kuoa na kuolewa,  wanahitaji kupewa uzito unaostahili. Na ndiyo kazi tunayofanya TaMCare kutoa ushauri nasaha ili kufanya kuwarejesha wanandoa katika hali ya kawaida,” amesema Dk. Mlyuka.

Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulilia Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Msangi, amesema ili matukio hayo yatokomezwe, Serikali itachukua  hatua za haraka  ikiwemo kutoa elimu kwa umma.

” Hili inabidi tuliseme ili watu wachukue hatua, kwa ajili ya kuokoa watoto wetu ambao wanathirika baada ya mfarakano au mauaji,” amesema Msangi.

Hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la mauaji ya wivu wa mapenzi. Ambapo Jeshi la Polisi Tanzania limesema katika kipindi cha Mei hadi Juni 2021,  kulikuwa na matukio ya mauaji ya wivu wa mapenzi 21.

error: Content is protected !!