Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Masheikh Uamsho wafutiwa mashtaka, DPP afunguka
Habari MchanganyikoTangulizi

Masheikh Uamsho wafutiwa mashtaka, DPP afunguka

Spread the love

 

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, amewafutia mashtaka viongozi 18 kati ya 36, wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, waliokuwa wanakabiliwa na makosa ya ugaidi, katika kesi ya jinai Na. 121/2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Masheikh hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi hiyo, kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, wamefutiwa mashtaka jana tarehe 15 Juni 2021.

Siku tatu baada ya kuzungumza na DPP Mwakitalu, tarehe 12 Juni mwaka huu, katika Mahabusu ya Gereza Kuu la Ukonga, walikokuwa wanashikiliwa.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu hatua hiyo, leo tarehe 16 Juni 2021, DPP Mwakitalu amesema amefuta mashtaka hayo, kwa kuwa mahakama hiyo ilikuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya masheikh hao.

“Unafahamu kwamba mahakama ilitoa uamuzi kwamba, makosa yaliyofanyika Zanzibar, Mahakama ya Tanzania Bara haina mamlaka, kwamba makosa yote yaliyofanyika Zanzibar, Mahakama Kuu ya Tanzania, haina mamlaka ya kuyasikiliza,” amesema DPP Mwakitalu.

DPP huyo mpya amesema “DPP hakuridhika na uamuzi huo, akaenda Mahakama ya Rufaa nayo ilitupa rufaa, ikisema kwamba haiwezi kukata rufaa kwenye maamuzi hayo madogo.”

Katika uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, uliotolewa tarehe 23 Aprili 2021, uliwafutia masheikh hao makosa 14 kati ya 25, yaliyokuwa yanawakabili, ambayo walikuwa wanadaiwa kuyafanya Zanzibar.

Hivyo, DPP Mwakitalu amesema, makosa 11 yaliyokuwa yamesalia, yalikuwa yanakosa nguvu na kupelekea ofisi yake kuyafuta.

“Kwa hiyo makosa yaliyofanyika , ambayo yalikuwa kwenye hati ya mashtaka yakiondolewa, makosa yanayobaki yanakosa nguvu. Kwa sababu hiyo, sisi tumefikia maamuzi kwamba tufute mashtaka yote,” amesema DPP Mwakitalu.

Aidha, DPP Mwakitalu amesema, Ofisi ya DPP Zanzibar kama itahitaji kuwafungulia mashtaka masheikh hao, itawafungulia kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar.

“Sababu washtakiwa walikuwa wako 36, lakini washtakiwa wengi hawakuwahi kabisa kufika Tanzania Bara, wakati ule makosa yanafanyika,”

“Kwa hiyo ni wachache walikuwa Tanzania Bara, kwa sababu hiyo, sisi tumefikia maamuzi kwamba tufute mashtaka yote. Halafu mamlaka za Zanzibar ikiona inafaa, basi tutawashtaki huko Zanzibar,” amesema DPP Mwakitalu.

Kuhusu washtakiwa wengine 18 waliobaki, DPP Mwakitalu amesema ofisi yake itapitia jalada zao na kwamba wakikutwa na tuhuma, wataunganishwa katika kesi zinazowahusu.

“ Lakini wale ambao wana makosa mengine tutawaungansiha kwenye kesi nyingine, lakini naendelea kufuatilia wale ambao walihusika kwenye makosa mengine, nikijiridhisha na makosa ambayo yamefanyika na kesi ziko pending mahakamani, tutaenda kuwaunganisha katika kesi zinazowagusa,” amesema DPP Mwakitalu.

Mkurugenzi huyo wa Mashtaka amesema, baadhi yao wataunganishwa katika kesi ya kuvamia Kituo cha Polisi Ushirombo, inayosikiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza.

“Kuna tukio lilitokea Ushirombo Kituo cha Polisi kilivamiwa, kwa hiyo baadhi wanahusika na kesi yao inasikilziwa Mahakama Kuu Mwanza. Hao tutawaunganisha kule tutaendelea nao na wengine wenye makosa mengine, tutawaunganisha kwenye kesi nyingine,” amesema DPP Mwakitalu.

Hadi sasa masheikh wawili, Mselemu Ally Mselemu na Farid Hadi Ahmed, wameachwa huru kutoka katika mahabusu ya Gereza Kuu la Ukonga, jijini Dare s Salaam, huku wengine wakitarajiwa kutoka katika nyakati tofauti.

Masheikh hao wameachwa huru baada ya kusota mahabusu kwa zaidi ya miaka minane, tangu walipokamatwa katika nyakati tofauti kati ya 2012 na 2014.

Masheikh hao walikuwa wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, walijihusisha na makosa ya ugaidi, kinyume na kifungu cha 27 (c), cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Watendaji Kata, Mitaa watakaoshindwa kusimamia usafi kukiona

Spread the love  WATENDAJI wa kata, mitaa na vitongoji na maofisa afya...

Habari Mchanganyiko

Mtia nia urais TLS kukata rufaa kupinga kuenguliwa

Spread the love  MTIA nia ya kugombea Urais wa Chama cha Mawakili...

Habari Mchanganyiko

NBC yazindua kampeni ya mkeka wa ushindi na ATM zake

Spread the loveBENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza uzinduzi wa kampeni...

Habari Mchanganyiko

Uholanzi wampongeza Rais Samia kuimarisha vyombo vya habari, demokrasia

Spread the love  UBALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania, umempongeza Rais Samia Suluhu...

error: Content is protected !!