April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mashambulizi Afrika Kusini: Tanzania yasitisha safari zake 

Spread the love

SERIKALI imesitisha safari za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwenda Afrika Kusini, kufuatia vurugu zinazoendelea nchini humo. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Raia wa taifa hilo, wamekuwa wakiwashambulia raia wageni wanaofanya shughuli mbalimbali nchini humo kwa madai, wanachukua kazi zao.

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 5 Septemba 2019 na Mhandisi Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mhandisi Kamwelwe amesema, ATCL limesitisha safari zake kwenda nchini humo hadi pale Tanzania itakapopokea taarifa za maandishi kutoka kwa Serikali ya Afrika Kusini, kuhusu hali ya usalama.

” ATCL imesitisha safari zake za nchini Afrika ya Kusini kufautia vurugu zinazoendelea nchini humo, mpaka pale ambapo Serikali ya Tanzania itapokea taarifa za kimaandishi kutoka kwa Serikali ya Afrika Kusini,” amesema Mhandisi Kamwelwe.

Wakati Tanzania kupitia ATCL ikisitisha safari zake, raia wa Nigeria waishio nchini Afrika Kusini wamepewa usafiri wa bure na serikali yao warudi nchini mwao, ili kujiokoa na mashambulio dhidi ya raia wa taifa hilo.

Geoffrey Onyeama, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria akizungumza na wanahabari tarehe 4 Septemba 2019 nchini humo, amesema kwa Wanaigeria waliotayari kurejea nchini mwao, wawasiliane na Tume Kuu ya nchi hiyo iliyoko mjini Pretoria au ofisi ya balozi Mkuu wa nchi hiyo jijijni Johannesburg, kwa ajili ya utaratibu zaidi.

Hata hivyo, Onyeama amesema hakuna raia wa Nigeria aliyepoteza maisha katika fujo hizo, na kueleza kwamba mamlaka husika zitadai fidia kwa mali za raia wake zilizoharibiwa katika shambulio hilo.

Wakati Nigeria ikitangaza uamuzi huo, nchi kadhaa zimetoa tamko kuhusu fujo hizo, ikiwemo Botswana ambayo imewataka raia wake kutofika maeneo yenye fujo.

error: Content is protected !!