July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe alianzisha; AG, Waitara wamtuliza

Spread the love

SUALA la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019, limeibuka bungeni na kusababisha mabishano baina ya Mwita Waitara, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mabishano hayo yaliibuka baada ya Mbowe kuhoji kama ni sahihi kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, kuanza kutumika pasipo kufikishwa bungeni kwa ajili ya kupitiwa na Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge.

“Inawezekana tukaona mambo haya ni mepesi mambo ya uchaguzi lakini amani ya taifa hili itapotea ama itaathirika kama tukipuuza masuala ya uchaguzi, Sheria ndogo zinazotungwa lazima zipitie bungeni, kabla hazijaanza kutumika kimsingi zinastahili kuletwa bungeni, vikao vya wadau vinavyokaa ni maoni, haviwezi kuwa mbadala wa bunge.

“Kamati ya sheria ndogondogo ya Bunge, haijawahi kuona au kupitia au kuthibitisha kuzikubali au kutoa maoni kuhusu kanuni zilizotungwa na TAMISEMI, ninachouliza mheshimiwa waziri atueleze katika utamaduni huo ambako tayari kanuni zimeingizwa kazini kamati ya sheria ndogo ndogo ya bunge haikuzipitia kwa kisingizio wadau wamezipitia na sio bunge je ni sahihi?” amehoji Mbowe.

Akimjibu Mbowe, Waitara amesema swali hilo linaonesha hofu ya wapinzani dhidi ya uchaguzi huo, huku akieleza kwamba kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 hazina upungufu wowote.

Waitara ameeleza, hofu ya wapinzani dhidi ya uchaguzi huo haina mashiko kwa madai kwamba, serikali imekuwa ikiendesha chaguzi mbalimbali nchini kwa uhuru na haki, na ndio maana wapinzani wengi wamekuwa wakichaguliwa katika nafasi mbalimbali.

“Hili swali ni  muhimu sana, hata swali la msingi la leo utaona ni  swali  lililojaa hofu bila sababu yoyote ile, kwasababu uchaguzi wa serikali za mitaa sio kwamba unaanza kufanyika kwa mara kwanza mwaka huu, ni uchaguzi tuliofanya miaka ya nyuma.

“Pia mimi nimekuwa mwenyekiti wa serikali za mitaa kupitia chadema chama cha upinzani, kama usingekuwa huru nisingekuwa mwenyekiti. Uchaguzi wa nchi hii ni huru, nilikuwa mbunge kupitia Chadema, na leo ninavyosimama ni mbunge wa CCM, hii inadhihirisha kama ni huru,” amesema Waitara.

Aidha, Waitara amesema kanuni hizo zimetolewa kwa vyama vya siasa vyote, na kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyelalamika kwamba kanuni hizo zina upungufu. Na kuwataka wapinzani kutowahofia wakuu wa wilaya na mikoa pamoja na wasimamizi wa uchaguzi huo.

“Waziri ametoa nakala za kanuni kwa wakuu wa mikoa wote na vyama vya siasa vyote vina kanuni, hakuna mtu amekuja mbele ya Watanzania akakosa kifungu chochote kama kina mapungufu, wamepokea wameridhia hakuna mapungufu.

“Tumeenda mbali zaidi, tumetoa muongozo kwa wapiga kura tumeeleza nani anastahili kugombea mchakato ndani ya vyama kusimamia uchaguzi. Nitashangaa watu wanakuja hapa wana hofu na wakuu wa mikoa watendaji,” amesema nakuongeza:

“Serikali imejipanga vizuri sana kuendesha uchaguzi wa serikali za mitaa na utasimiwa na waziri mwenye dhamana Watanzania wako tayari kufanya uchaguzi wa haki ili kupata viongozi wao.”

Waitara amesema, Wananchi wasiwe na hofu uchaguzi utasiamiwa na vyombo vipo, na yeyote mwenye maelezo ofisi ya tamiemi iko wazi wanakaribisha maoni.

Dk. Adeladius Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali  amesema, si sahihi kwamba sheria ndogo zinapotungwa lazima zijadiliwe bungeni, bali taratibu zinaelekeza kanuni hizo ziwasilishwe katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa ajili ya kuchambuliwa.

Dk. Kilangi amesema, baada ya sheria hizo kuchambuliwa na Ofisi ya AG,  waziri husika hutangaza sheria hiyo katika gazeti la serikali kisha huanza kutumika.

“Naomba nitoe maelezo kidogo kuhusu suala ambalo ameliibua mheshimiwa Mbowe, amesema kwamba sheria ndogo ndogo  zinapotungwa lazima ziletwe bungeni kabla ya kutumika, hivyo kwa mujibu wa utaratibu sio sahihi,” amesema Dk. Kilangi na kuongeza;

“Niongeze kusema mtu anaweza kusema labda mchakato huo hautoi nafasi ya kuziangalia vizuri sheria ndogo, kimsingi hutungwa chini ya sheria mama na ipo misingi ya kisheria inayoeleza namna gani sheria ndogo itungwe na moja wapo ya misingi hiyo ni kwamba isipingane kimsingi na sheria mama, inapotokea changamoto kamati hutoa maoni na maelekezo yake na kama kuna changamoto zinarekebishwa.”

error: Content is protected !!