May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa awanyooshea kidole wanufaika mikopo elimu ya juu

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewataka wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu nchini humo, ambao bado hawajajitokeza na kuanza kurejesha, wafanye hivyo mara moja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea)

Pia, amewataka waajiri wote nchini Tanzania, katika sekta binafsi na sekta ya umma, watoe kipaumbele kwa makato ya mikopo ya elimu ya juu kama yalivyo makato mengine ya kisheria.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumamosi, tarehe 13 Februari 2021, wakati akiahirisha mkutano wa Pili wa Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma, had0 Jumanne 30 Machi 2021 saa 3:00 asubuhi, litakapokutana tena.

Amesema mikopo ya elimu ya juu, kwa mwaka huu 2020/2021, serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 55,287 na akisisitiza kwamba, wataendelea kuzingatia kigezo pekee cha uhitaji wa mwombaji sanjari na kurahisisha matumizi ya mtandao katika uombaji na utoaji wa mikopo.

Majaliwa amesema, katika kuongeza ufanisi wa utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, serikali imefanya maboresho ya kisheria, kimfumo na kiutendaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015/2016 – 2019/2020).

Waziri mkuu amesema, matunda ya maboresho hayo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo ya fedha za mikopo kutoka wastani wa shilingi 28.9 bilioni mwaka 2016/2017 hadi kufikia wastani wa shilingi 192 bilioni mwaka 2019/2020.

Wairi Mkuu akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

“Serikalini inafarijika na inapokea kwa mikono miwili michango yenye afya na tija kuhusu hatma ya mikopo inayotolewa na serikali baada ya miaka 15 ya uwepo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na ipo tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kuhusu namna bora zaidi ya kuufanya mfuko huu.”

Amesema ili mfuko huo uwe endelevu na himilivu na wenye manufaa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa huku akiagiza wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuboresha huduma zake na kurahisisha urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika waliojiari katika sekta binafsi.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuzungumza ukusanyaji wa mapato akisema, Serikali itatekeleza mikakati mahususi ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ambayo ni pamoja na kukasimisha jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa Halmashauri na serikali za mitaa.

Amesema, serikali itaimarisha ushirikiano kati ya mamlaka zinazokusanya mapato na vyombo vya ulinzi na usalama katika kufanya doria maeneo ya mipaka ya nchi kavu, baharini na kwenye maziwa ili kudhibiti biashara za magendo.

“Pia Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi kwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanatumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD),” amesema Majaliwa

error: Content is protected !!