Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Tangulizi Mahakama ya ICC yapata mwendesha mashtaka mpya
Tangulizi

Mahakama ya ICC yapata mwendesha mashtaka mpya

Karim Khan
Spread the love

 

NCHI wanachama wa mkataba wa Roma ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu dhidi ya binadamu (ICC), umemchagua mwanasheria kutoka Uingereza, Karim Khan kuwa mwendesha mashtaka mpya wa mahakama hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Khan anachukua nafasi ya Fatou Bensouda, anayetarajiwa kumaliza muhula wake wa utumishi wa miaka tisa katika mahakama hiyo, tarehe 15 Juni 2021.

Bensouda raia wa Gambia ameiongoza mahakama ya The Hague, kwa mafanikio makubwa na kuweka rekodi ya kuendesha uchunguzi kuanzia mzozo wa mwaka 2014 kati ya Israel na Palestina, katika ukingo wa Gaza hadi Afghanistan.

Anaondoka madarakani akiwa amevuna heshima kubwa ulimwenguni. Miongoni mwa mafanikio yake, ni pamoja na kuibadilisha ICC kutoka kushughulikia migogoro ya Afrika, hadi ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani na washirika wake wengine ulimwenguni.

Mwaka uliyopita, Bensouda aliwekewa vikwazo na aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kutokana na hatua yake ya kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa nchini Afghanistan, ukiwahusisha pia wanajeshi wa Marekani.

Aidha, taifa hilo lilibatilisha kibali cha kusafiria cha Bensouda, kufuatia hofu kuwa ataanzisha uchunguzi dhidi ya wanajeshi wa Marekani wanaotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.

Hata hivyo, mwendesha mashitaka wa ICC, alieleza kuwa ataendelea na majukumu yake bila uwoga au fadhila kutoka kwa mtu yeyote, na kwamba uamuzi huo wa Marekani, hautaathiri kazi zake.

Bensouda amekuwa akichunguza madai ya uhalifu wa kivita kwenye mgogoro wa Afghanistan kuanzia Novemba mwaka 2017, ikiwemo uwezekano wa jukumu la watumishi wa Marekani, kuhusiana na kufungwa kwa washukiwa.

Katika uchaguzi huo, wagombea wanne Khan (Uingereza), Carlos Castresana (Uhispania), Fergal Gaynor (Ireland) na Francesco Lo Voi (Italia), walijitosa kumrithi mwanamama huyo shupavu ulimwenguni.

Khan ambaye amejikita katika sheria ya kimataifa na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, alibuka mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi huo wa siri na kuhitimisha mchakato huo mgumu wa kutafuta mrithi wa Bensouda.

Fatou Bensouda

ICC ni mahakama pekee ya kudumu inayoendesha kesi za uhalifu wa kivita duniani, baada ya miaka kadhaa ya kuminywa upatikanaji wa haki kwa ukatili uliofanywa kwenye nchi kama Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia.

Bensouda alichaguliwa rasmi kushika nafasi hiyo, Juni 15 2012, kutoka kwa Luis Moreno-Ocampo, raia wa Argentina.

Kabla ya kuteuliwa kuwa mwendesha mashitaka wa ICC, Bensouda alikuwa Makamu Muendesha Mashitaka wa mahakama hiyo, kati ya mwaka 2004 hadi 2012.

Vilevile, Bensouda amewahi kuwa mwanasheria mkuu na waziri wa haki nchini Gambia. Ana shahada ya uzamili wa Sheria ya Kimataifa ya Shughuli za Baharini.

Katika ripoti yake ya Novemba mwaka jana, Bensouda alisema, kwa uchache kuna visa 61 vilivyorikodiwa, ambapo matukio ya utesaji, ukatili na kuvunja heshima ya watu vinaonekana kutendeka.

Ripoti hiyo pia inataja visa vingine 27 vya watu walioteswa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), vingi kati ya visa hivyo, vikitendeka kati ya mwaka 2003 na 2004.

Anasema, uhalifu ulitendeka haukuwa matukio yaliyojitenga, bali ni sehemu ya mbinu zilizoratibiwa na Marekani katika kujaribu kupata taarifa kutoka kwa mahabusu.

“Kuna ushahidi wa kutosha kuamini kuwa uhalifu huu ulitendeteka katika kuendeleza sera ya kupata taarifa kupitia matumizi ya mbinu za mahojiano zinazojumuisha njia za kikatili au fujo, ambazo zingelisaidia malengo ya Marekani nchini Afghanistan,” Bensouda ameeleza katika ripoti hiyo yake.

Miaka kadhaa iliyopita, Bensouda amejaribu kupanua wigo wake, kutoka kuilenga Afrika, na kuhusisha mataifa kama Afghanistan, Palestina, ambayo ni mwanachama wa mkataba wa Roma na Georgia.

Kabla ya hatua hiyo, na hatua ya Marekani, Urusi na China kukataa kuwa wanachama wa ICC, mahakama hiyo imekuwa ikikosolewa kushughulikia migogoro ya mataifa maskini ya Afrika.

Pamoja na kwamba Khan alitazamwa na wengi kama mtu mwenye nafasi kubwa ya kushinda nafasi hiyo, lakini hakuweza kupata kupata uungwaji mkono wa kutosha katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Duru ya pili ya uchaguzi, ulifanyika Ijumaa katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), nchini Marekani.

Makamu wa rais wa baraza la mataifa wanachama, Michal Mlynar, alipomtangaza Khan kuwa mshindi, makofi kidogo yalisikika katika ukumbi, ambako wanadiplomasia waliokuwa wamevaa barakoa walipiga kura mmoja baada ya mwingine, huku wakitumbukiza kura zao kwenye maboksi yalioweka mbalimbali kutokana na tishio la maambukizi ya virusi vya COVID-19.

Khan alipata kura 72, nyingi kabisa kuliko zilizohitajika, huku mshindani wake wa karibu, raia wa Ireland, Fergal Gaynor, akishika nafasi ya pili kwa kuambulia kura 42.

Naye Mhispania Carlos Castresana Fernandez, alipata kura 5 na hivyo kushika nafasi ya tatu, huku Mtaliano, Francesco Lo Voi, akishika mkia kwa kupata kura 3. Mwanachama mmoja hakupiga kura.

Kwa sasa, Khan anaongoza timu ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa kuchunguza madai ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kutekelezwa na kundi linalojiita “Dola la Kiislamu nchini Iraq.”

Mbali na jukumu hilo, Khan anashikilia cheo cha katibu mkuu msaidizi wa umoja wa mataifa (UN).

Amefanya kazi kama mwendesha mashtaka wa mahakama inayoshughulikia uhalifu wa kivita katika Yugoslavia ya zamani, na uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Ndani ya ICC siyo mgeni. Aliwahi kuwa wakili wa utetezi wa naibu rais wa Kenya, William Ruto Kwa upande mwingine wakili wa aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma, Francis Muthaura.

na aliweza kushawishi majaji wa mahakama hiyo, kutupilia mbali kesi dhidi ya Rutto na wenzake.

Katika kesi hiyo, Khan aliweza kuwashawishi majaji wa ICC, kutupilia mbali kesi dhidi ya Rutto na wenzake; hoja ambazo zilimsukuma mmwendesha mashitaka kuomba kuliondoa shauri hadi utakapopatikana ushahidi mpya.

Khan amewahi pia kulihudumu kama mwanasheria wa Seif al-Islam Gadhafi, mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Moammar Gadhafi, ambaye mpaka leo bado anatafutwa na ICC kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mkataba wa Roma ambao ndiyo umeanzisha mahakama ya ICC, ulisainiwa 17 Julai 1998 na mahakama hiyo ilianza shughuli zake, tarehe 1 Julai 2002, ikiwa na mamlaka ya kuendesha kesi za uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya Kimbari.

Hata hivyo, mahakama hiyo, inaingilia kati masuala hayo, pale inapojiridha kuwa mahakama za ndani zimeshindwa kuanzisha uchunguzi wa mashtaka hayo.

Wanachama wake 123 wanafungamanishwa na vipengele vyake, ambavyo vinajumlisha kukamata watu wote wanaotafutwa na mahakama hiyo.

Akizungumzia kuchaguliwa kwa Khan, mkurugenzi wa haki ya kimataifa wa shirika la Human Rights Watch, Richard Dicker amesema, “Khan amechaguliwa katika wakati ambapo ICC inahitajika zaidi kuliko ilivyowahi kutokea, lakini ikiwa inakabiliwa na matatizo makubwa na shinikizo kuhusu jukumu lake.”

Amesema, “tutamtegemea bwana Khan kushughulikia kasoro za kiutendaji za mahakama hiyo, huku akionesha uhuru thabiti katika kutafuta kuwawajibisha hata wakiukaji wa haki wenye nguvu zaidi.”

Wakati Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limetumia madaraka yake chini mkataba wa Roma kuipeleka mizozo ya Darfu Magharibi nchini Sudan na Libya katika ICC, miito kwa chombo hicho chenye nguvu zaidi kuipeleka Syria, na hivi karibuni zaidi Myanmar katika mahakama hiyo bado haijafanikiwa.

Dicker alisema, “mahakama hiyo katika miaka 18 imejitanabahisha kama anuani ya kudumu kwa uwajibikaji kwa makosa mengi makubwa.”

Majuzi, majaji wa ICC waliikasirisha Israel kwa kusema mamlaka ya mahakama hiyo yanakwenda hadi kwenye maeneo yanayokaliwa na nchi hiyo, tangu vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, jambo ambalo linaweka uwezekano wa mwendesha mashtaka kufungua uchunguzi juu ya vitendo vya jeshi la Israel na ujenzi wa makaazi ya walowezi katika eneo na Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!