Sunday , 29 January 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Majaliwa atoa maagizo kwa sekta binafsi Tanzania
Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Majaliwa atoa maagizo kwa sekta binafsi Tanzania

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka sekta binafsi iweke kipaumbele na kuzingatia usawa wa kijinsia katika utoaji wa ajira hasa wanawake ili kuunga mkono jitihada za Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, katika mwaka 2020/2021, ukosefu wa ajira kwa wanawake upo juu zaidi ikilinganishwa na wanaume ambapo wanawake wasiokuwa na ajira wanafikia asilimia 12.7 ilhali wanaume ni asilimia 5.8.

Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema hayo jana Jumamosi, tarehe 4 Desemba 2021, katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Jumuia ya Watendaji Wakuu wa Makampuni na Mashirika (CEO Roundtable of Tanzania), jijini Dar es Salaam.

“Katika mipango yenu ya sasa na baadaye, toeni kipaumbele kwenye mikakati ya kuwainua wanawake katika shughuli za uchumi na hivyo, kumuunga mkono kwa vitendo Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye maeneo mbalimbali nchini,” amesema Majaliwa

Aidha, Majaliwa aliipongeza sekta binafsi kwa namna inavyoshiriki katika kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa Watanzania kupitia makampuni na mashirika mbalimbali nchini.

Alisema moja ya mafanikio makubwa ni kuongezeka kwa ajira kutoka ajira milioni 20.5 mwaka 2014 hadi ajira milioni 24.1 mwaka 2020/2021 na kuongezeka kwa ajira kwenye sekta isiyo rasmi kutoka asilimia 22.0 mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka 2020/2021.

Alisema licha ya changamoto ya UVIKO-19, Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwenye sekta nyingine za kiuchumi na kutoa ajira katika sekta ya kilimo, hali ambayo inaashiria mwelekeo mzuri katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaolenga kuwa na asilimia 60 ya ajira kwenye kilimo ifikapo mwaka 2025/2026.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uwekezaji, biashara na kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hatua hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji nchini hususan kutoka nje ambao kati ya Machi na Agosti, 2021 ulifikia takriban dola za Marekani bilioni tatu.”

Waziri Mkuu alisema Rais Samia ameendelea kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara na anaamini kupitia mkutano huo watatoa ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji.

Aliongeza Serikali ina matarajio na sekta binafsi kuwa itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na kupunguza hewa ya ukaa na matumizi ya plastiki.

“Ongezeni uwekezaji kwenye miradi ya matumizi ya nishati mbadala, ustawishaji wa misitu na utunzaji wa mazingira na usafirishaji kwa kutumia teknolojia za kisasa zisizozalisha hewa ya ukaa,” alisema na kuongeza:

“Nitoe wito kwenu muendelee kuwaita wawekezaji waje hapa nchini na kuwekeza katika sekta mbalimbali za kilimo, utalii na nishati.”

Naye, Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania, Sanjay Rughani aliipongeza Serikali kwa namna inavyoshirikiana na sekta binafsi katika kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa watahakikisha kupitia shughuli zao, wanaifanya Tanzania ikue kiuchumi siyo tu Afrika bali duniani kwa ujumla.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Huawei Tanzania yatajwa miongoni mwa waajiri bora kimataifa

Spread the loveKAMPUNI ya Huawei Tanzania imetajwa kuwa mwajiri bora nchini na...

Habari Mchanganyiko

Waziri wa uchumi wa Finland atua nchini, kuteta na mawaziri 7

Spread the loveWAZIRI wa Masuala ya Uchumi wa Finland, Mika Tapani Lintilä...

Habari Mchanganyiko

Asimilia 79 wafeli somo la hesabu matokeo kidato cha nne

Spread the loveWATAHINIWA wa shule 415,844 sawa na asilimia 79.92 ya watahiniwa...

Habari Mchanganyiko

NECTA yafuta matokeo ya watahiniwa 333 kwa kuandika matusi, kudanganya, 286 yazuiwa

Spread the loveBARAZA la Mitihani la Tanzania (Necta) leo Jumapili limetangaza kuyafuta...

error: Content is protected !!