January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Baraza Vyama vya Siasa: Tanzania ina katiba nzuri, bunge huru

Spread the love

 

BARAZA la Vyama vya Siasa, limezungumzia miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, likisema nchi ina Katiba nzuri, pamoja na mihimili iliyo huru. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 4 Desemba 2021 na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib, akizungumzia mafanikio ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, yanayotarajiwa kufanyika tarehe 9 Desemba mwaka huu.

Taarifa ya mwenyekiti huyo wa Baraza la Vyama vya Siasa, imesema Katiba iliyopo inatoa haki za kidemokrasia na kisiasa kwa kila mtu.

“Tanzania ni nchi huru na tumefanikiwa kulinda uhuru wetu kama tulivyoeleza hapo awali. Hivyo, tunawaasa wananchi wote ikiwamo vyama vya siasa, tuendelee kulinda uhuru wetu. Tanzania huru ina Katiba nzuri inayotoa haki za kidemokrasia na kisiasa kwa kila mtu, ambapo vyama vya siasa vinaandikishwa na kufanya shughuli zake kwa uhuru unaohitajika,” imesema taarufa hiyo.

Taarifa hiyo imesema kuwa, Bunge na Mahakama viko huru katika utekelezaji wa majukumi yake.

“Kuna vyombo vya haki na kidemokrasia kama Bunge, Mahakama na vyombo vya habari, ambavyo Vipo huru na vinafanya kazi kwa weledi na haviingiliwi na mtu au taasisi yoyote. Hivyo, tunaomba jumuiya ya kimataifa, ishirikiane nasi kudumisha uhuru na utashi wetu, na asitokee mtu au taasisi au nchi ya kutupangia kitu cha kufanya kwani kila nchi ina mambo yake,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema”Nchi yetu imeendelea sana katika masuala ya demokrasia na siasa na ni mojawapo wa mifano ya kuigwa dunia. Mojawapo ya masuala makubwa tuliyofanikiwa katika demokrasia na siasa, ni kuendesha mfumo wa demokrasia uliokuwapo na uliuopo sasa, katika hali ya amani, utulivu, uzalendo, kimaadili na umoja wa kitaifa, huku tukilinda uhuru wetu. Haya ni mafanikio makubwa ambayo nchi nyingi zimeshindwa kuyapata kama ilivyo sisi. Hivyo, tuna haki ya kujivunia na kuyadumisha. Changamoto zipo, lakini ni zile zinazozungumzika na kutalitulika.”

Aidha, Mhatib kupitia taarifa hiyo, ameviomba vyama vya siasa kulitumia baraza hilo katika kutafuta suluhu ya changamoto zao.

“Katika nchi yetu pia kuna Baraza la Vyama vya Siasa, ambalo linakutanisha viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa vyote vyenye usajili kamili. Katika baraza tunajadili masuala mbalimbali yanayotuhusu vyama vya siasa na kama kuna changamoto tunazijadili na wahusika ili kupata ufumbuzi,” imesema taarifa ya Khatib na kuongeza:

” Hivyo, ni sehemu nzuri na muafaka kwa vyama vya siasa kubadilishana mawazo na kujadili changamoto zinazojitokeza, kuliko kwenda kuongelea changamoto hizo katika vyombo vya habari au sehemu nyingine ambazo muhusika hana nafasi ya kuzijadili ili kupata ufumbuzi wake.”

error: Content is protected !!