Thursday , 23 March 2023
Home Kitengo Maisha Afya Maambukizi ya corona: Taifa njia panda
AfyaHabari za SiasaTangulizi

Maambukizi ya corona: Taifa njia panda

Spread the love

 

MKANG’ANYIKO wa taarifa juu ya virusi hatari vya corona (Covid-19), nchini Tanzania, unazidi kuwaweka wananchi njia panda. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mkanganyiko wa sasa, unatokana na maoni yenye taswira mbili tofauti – Serikali kwa upande mmoja na viongozi wa madhehebu ya kidini na baadhi ya wanasiasa wa upinzani kwa upande mwingine.

Akizungumza kutoka Chato, mkoani Geita, jana Jumatano, tarehe 27 Januari 2021, Rais John Magufuli alisema, “…muendelee kuchukua tahadhari,” lakini “msitishwe.”

Alikuwa akizindua shamba la miti lililopewa jina la Msitu wa Silayo, wilayani Chato.

Akaongeza, “katika kipindi hiki magonjwa yanayojitokezatokeza, yasiyojulikana kama corona, nchi nyingi wananchi wake watakuwa wamejifungia ndani. Sisi hatujajifungia na hatutegemei kujifungia.”

“Wala sitegemei kutangaza hata siku moja kwamba tunajifungia ndani, kwa sababu Mungu wetu yuko hai na ataendelea kutulinda.”

Alisema, “kuna Watanzania waliokimbilia maeneo mengine na kwenda kuchanjwa na walipochanjwa huko, wamekuja huku na kutuletea corona ya ajabu ajabu. Simameni imara, chanjo hazifai.”

Akawataka wananchi kuwa waangalifu kwa kile alichoita, “mambo ya kuletewa letewa,” na kuongeza, “Watanzania msifikirie mnapendwa sana na mataifa ya nje.”

Akaelekeza wizara ya afya kutokimbilia chanjo kutoka nje bila kujiridhisha.

Alidai kuwa kuna nchi ambayo haikutaja, walipelekewa chanjo ya kansa ya kizazi, ingawa baadaye ikaonekana ni chanjo ya kuzuia kuzaa.

Hata hivyo, Askofu Mkuu Mwandamizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi anasema, “corona haijaisha. Bado ipo. Tusali na tujiombee sisi wenyewe, ili Mungu atulinde na janga la Covid-19.”

Askofu Ruwa’ichi alitoa kauli hiyo, katika kuadhimisha Misa Takatifu ya Kumbukumbu ya Wafia Dini, iliyofanyika katika kituo cha Hija Pungu, Ilala jijini Dar es Salaam.

Askofu Isaac Aman, wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha

Amesema, “tusiende holela. Tuwe makini na tujilinde. Utamaduni wa barakoa tuliouacha, tuurudie tena. Tujijali, tujipende, tujitunze, tushirikiane na Mungu katika kujilinda na tuendelee kuomba ulinzi kwa ajili yetu sote.”

Akawataka waumini wa kanisa hilo, kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Naye Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Aman ameeleza wiki iliyopita, kwamba “…tusimjaribu Mungu kwa kufanya uzembe na maisha yetu. Turejee na tahadhari za kuzuia maambukizi bila ya kuwa na hofu.”

Alisema hayo kupitia waraka wake alioutoa kwa umma na kusomwa kwenye makanisa yaliyopo kwenye jimbo lake, Jumapili iliyopita ya tarehe 24 Januari 2021.

Waraka wa Askofu Amani umepewa kichwa cha maneno kisemacho: “Kutembea Pekupeku Juu ya Mbigili.”

Akiwataka waumini wake kutomjaribu Mungu, Askofu Amani alisema, “tusipuuze sharti la kujikinga na maambukizi ya virusi vya Korona. Watu wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa ugonjwa huo upo na unatesa mataifa mengi duniani.”

Alisema, “maji ya kunawa kanisani yameondolewa, na pengine yapo lakini watu hawanawi tena kwa imani kwamba hakuna corona. Hata ile tahadhari ya kutoshikana mikono watu wamejiondolea wenyewe kwa imani kwamba, hakuna corona,…mwenendo wake wa sasa, unatia mashaka.”

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga ameandikia barua Mwadhama, Mpelekwa wa Baba Mtakatifu, Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Maaskofu Wastaafu akiwataka kuchukua tahadhari ya maambukizi mapya ya Korona.

Barua ya rais huyo wa TEC kwenda kwa viongozi hao, ilitumwa tarehe 26 Januari 2021 na kupewa kichwa cha maneno kisemacho, “tahadhari juu ya maambukizi mapya ya virusi vya Korona na ugonjwa wa Uviko 19 (COVID 19.”

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga

Nyaisonga ni Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya.

Alisema, kuna wimbi jipya la maambukizo ya Korona kufuatia nchi kadhaa kuthibitisha kupita kwenye kipindi kigumu cha kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.

Waraka wa TEC kwenda kwa maakofu umerekodiwa kwa kupewa kumbu Na. TEC/PR/2021/02 la tarehe 26 Januari mwaka huu.

Amesema, “nchi yetu siyo kisiwa. Hatuna budi kuzingatia hekima ya wahenga wanasema, mwenzio akinyolewa wewe wewe tia maji. Ni muhimu tukaendelea kuzingatia kanuni za afya katika kukohoa au kupiga chafya na kuepuka kusogeleana, kugusana na kusongamana.”

Anasema, “hatuna budi kujihami, kuchukua tahadhari na kumlilia Mungu kwa nguvu zaidi, ili janga hili lisitukumbe.”

James Francis Mbatia, mwenyekiti wa taifa wa chama cha siasa cha NCCR- Mageuzi, naye hakuwa nyuma, katika kuzungumzia janga hili.

Akizungumza na waandishi wa habari, Jumatano, makao makuu ya chama chake, Ilala, jijini Dar es Salaam, mwanasiasa huyo ambaye amepata kuwa mbunge wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro, kwa miaka 10 alitaka wananchi kuchukua tahadhari ya kukabiliana na maambukizi.

“Taarifa za kidunia zinaonyesha, virusi vipya vya ugonjwa huu wa Korona kutoka Afrika Kusini, Brazil na Ulaya, maambukizi yake yameongezeka kutoka asilimia 30 mpaka 70, hivyo hatuna budi kujingika kwa kila Mtanzania,” ameeleza.

Amesema, “ni wajibu wetu sote kulinda uhai wetu kwa gharama yoyote kwa kuwa ni janga la kidunia. Tuondoke gizani kwa kila mtu kuchukua tahadhari kwa kuwa kila mtu ana haki ya kuishi…”

Mbatia amesema, “suala la uhai, ni jambo la mtu binafsi. Hatuhitaji kibari cha serikali katika kujilinda kwenye jambo hili.”

Wakati serikali ikipata kigugumizi cha kueleza moja kwa moja kuwapo kwa ugonjwa huo nchini, katika baadhi ya ofisi za umma na binafsi, kumewekwa tahadhari, ikiwamo maji ya kunawa mikono na madawa.

Aidha, katika baadhi ya ofisi za serikali, mabenki na hospitali za serikali, mgeni asiyevaa barakoa, haruhusiwi kuingia ndani ya ofisi hizo kupata huduma.

Mfano wa karibu kabisa, ni makao makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, ofisi za msajili wa vyama vya siasa mjini Dodoma, wizara ya fedha, NMB benki na hospitali ya Muhimbili.

Baadhi ya vituo vya mabasi ya mwendokasi cha kivukoni, jijini Dar es Salaama, wamerejesha utaratibu wa kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka kwenye mabomba na sabuni kwa abiria wanaotumia usafiri huo.

Hata hivyo, kituoni hapo hakuna kiongozi anayesimamia utaratibu huo bali abiria wanatekeleza utaratibu huo wao wenyewe ambapo wapo wanaonawa na wengine hawafanyi hivyo.

2 Comments

  • Natoa pongezi kwa maaskofu waliojitokeza na kutahadharisha kuwa haitoshi kumuomba Mungu peke yake, Ni vizuri na wakuu wa dini nyingine wakajitokeza pamoja na wataalamu wetu

  • Hivi Maalim Seif akiwa hospitali anatibiwa kwa kufukizwa au kwa madawa ya wazungu?
    Kama kufukiza kwa nini asikae nyumbani tu akaendelea kujifukiza?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

AfyaHabari

Ugonjwa wa ajabu ulioua watano Bukoka ni Marburg

Spread the loveWAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa ajabu uliosababisha...

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

AfyaHabariHabari

Ugonjwa wa ajabu wadaiwa kuua watano Kagera, Serikali yatoa tahadhari

Spread the loveJUMLA ya watu watano wanaidaiwa kufariki dunia  katika vijiji vya...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

error: Content is protected !!