December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ziara ya JPM: DED Kahama anusurika, aipandisha hadhi

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba (aliyesimama) akimshukuru Rais Magufuli kwa kumsamehe

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amemsamehe kumfuta kazi, Anderson Msumba, Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga aliyetuhumiwa kununua gari kinyume cha sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga…(endelea).

Msumba alikuwa anatuhumiwa kununua gari lenye thamani ya Sh. 400 Milioni kinyume cha sheria ambapo mwishoni mwa mwaka 2020, Rais Magufuli alimuagiza Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Seleman Jaffo amfukuze kazi sambamba na kumpokonya gari hilo.

Leo Alhamisi tarehe 28 Januari 2021, akizungumza na wanahanchi wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga, Rais Magufuli amesema, ameamua kumsamehe mkurugenzi huyo kutokana kuridhishwa na utendaji kazi wake.

Hata hivyo, Rais Magufuli amempa angalizo mkurugenzi huyo la kutorudia tena kwenda kinyume cha sheria.

“Nimeamua kumsamehe mkurugenzi huyu na hili gari ninamrudishia aendelee kuliendesha, lakini asirudie tena kununua gari nje ya utaratibu wa sheria,” amesema Rais Magufuli.

Akielezea utendaji kazi wa Msumba, Rais Magufuli amesema, amefanikiwa kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya halamshauri hiyo.

“Nikaambiwa fedha zote ni mapato ya ndani ya halmashauri hii, nikawa namuangalia mkurugenzi alikuwa na kituhuma tuhuma cha kujinunulia gari, nikasema lakini kama fedha na kupitia madiwani wamejenga hili jengo la Sh.1.8 bilioni. Wanajenga jengo la hospitali kubwa la Sh.3 bilioni, ” amesema Rais Magufuli.

Akiendelea kumsifu mkurugenzi huyo, Rais Magufuli amesema, kwa kushirikiana na madiwani, amewezesha ujenzi wa kiwanda kikubwa, baada ya kutoa eneo la hekari 90 bure kwa muwekezaji.

“Ngoja nione mpaka mwisho nikapelekwa kwenye mradi wa tatu nikakuta likiwanda likubwa, kama yale maviwanda nilikuwa nayaona Ulaya.

“Nilipo kuwa nikipewa taarifa pale, nikaambiwa ardhi hii yote ilitolewa na halmashauri na ni heka 90 lilitolewa bure, nikajiuliza sana huyu mkurugenzi na madiwnai wana akili sana, wametoa eneo bure hawakumuuzia yule muwekezaji,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, uamuzi huo wa Msumba na madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, utasaidia kuongeza mzunguko wa fedha pamoja na kutoa nafasi za ajira pindi kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi.

“Lengo lao wameangalia mbele zaidi kwamba wakishajenga kiwanda, kwanza kitatengeneza jira za wananchi wa hapa, lakini watakusanya kodi, ukishatengeneza ajira ukakusanya kodi, ukaongeza mzunguko wa fedha ,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, utendaji kazi huo wa Msumba umefuta makosa yake.

“Kakosa kale kadogo kamefuta dhambi zake, nimeshangaa kweli kwamba wilaya hii ya Kahama ina mipango mikubwa ninayoipenda,” amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameipandisha hadhi Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga kuwa Manispaa, baada ya kuridhishwa na maendeleo yake ikiwemo ukusanyaji mapato.

“Nimeshangaa Wilaya ya Kahama ina mipango mikubwa ninayopenda, kwa sababu mmenipa kura, ndio rais na kazi yangu ni kupandisha, nina ipandisha iwe manispaa,” amesema Rais Magufuli.

Amesema, Halmashauri ya Mji wa Kahama inachangia asilimia 50 ya mapato ya Mkoa wa Shinyanga.

“Hata makusanyo ya mapato ni miongoni mwa halamshauri chache zinazoongoza katika makusanyo, lakini hata kura mlinipa nyingi,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!