Sunday , 30 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ‘Local content’ inavyotajirisha Watanzania, wavuna mabilioni
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Local content’ inavyotajirisha Watanzania, wavuna mabilioni

Spread the love

Ushirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za madini (Local Content) na Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) ni moja ya mambo ambayo yamekuwa yakipigiwa chapuo na Serikali kupitia wizara ya madini ili Watanzania wanufaike na rasilimali zao.

Mathalani katika ya Sheria ya madini ya mwaka 2017/2018 iliyoboreshwa mwaka 2019 na kisha kuongezwa kanuni ya ushirikishwaji wazawa (Local Content), mafanikio ya maboresho hayo yameanza kuonekana kwa kuwezesha Watanzania kuvuna mabilioni kutokana na mauzo ya bidhaa na huduma wanazotoa kwa kampuni kubwa za madini nchini.

Hayo yamedhihirishwa hivi karibuni katika hotuba ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliyoiwasilisha bungeni kuomba Bunge liidhinishe kiasi cha Sh bilioni 231.9 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Katika bajeti hiyo aliyoptishwa bungeni jijini Dodoma, Mavunde anasema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Wizara kupitia Tume ya Madini ilipokea na kupitia jumla ya mipango 801 ya ushirikishwaji wa Watanzania katika shughuli za madini ambapo mipango 797 iliidhinishwa na mipango minne haikukidhi vigezo hivyo wahusika walitakiwa kufanya marekebisho stahiki.

Aidha, anasema Wizara kupitia Tume ya Madini ilipokea na kuchambua maombi ya vibali vya ununuzi 154 kutoka katika migodi ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Bulyanhulu Gold Mine Limited, North Mara Gold Mine Limited, Shanta Mining Company Limited, Lindi Jumbo Limited, Buckreef Gold Company Limited, Mamba Corporation Limited, Tembo Nickel, Mantra Tanzania Limited, Zeus Resources na AUMS Tanzania Limited.

Pia, maombi 447 ya ununuzi wa bidhaa na huduma (local content) yalipokelewa na kuidhinishwa kisha kupata kibali cha ununuzi.

“Katika mwaka 2023 kampuni za kitanzania ziliuza migodini bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.48 ambayo ni sawa na asilimia 90 ya mauzo yote yaliyofanyika migodini yenye thamani ya dola za Marekeni bilioni 1.65.

Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa (katikati) alipotembelea banda la maonyesho la GGML katika Kongamano la tatu la uzingatiaji wa ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) Mei 2024. Kutoka kushoto kwenda kulia ni Dominic Marandu, Meneja wa Mafunzo na Maendeleo wa GGML, Rhoda Lugazia, Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa GGML, David Nzaligo, Mwanasheria mwandamizi wa GGML na Gilbert Mworia, Meneja Mwandamizi wa GGML anayeshughulia mahusiano endelevu.

“Mauzo hayo yaliyofanywa na kampuni za wazawa kwa mwaka 2023 yalikuwa ni zaidi ya mauzo yaliyofanywa mwaka 2022 ambayo yalikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 713 sawa na asilimia 82 ya mauzo yote ya dola za Marekani milioni 874 kwa mwaka huo,” anasema na kuongeza;

“Napenda kutumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwahamasisha  watanzania kuchangamkia fursa ya kuanzisha viwanda vya kuzalisha vifaa pamoja na bidhaa mbalimbali zinazotumika migodini.”

Mojawapo ya kampuni ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuzingatia kanuni hizo za kushirikisha wazawa kwenye sekta ya madini (Local content) ni Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti.

Kampuni hiyo pia imetajwa kuwa mfano bora wa uwajibikaji kwa jamii pamoja na kuzingatia kanuni hizo za Local content na kuboresha maisha ya watu wanaozunguka mgodi huo. Mbali na uwajibikaji wa kampuni hiyo kwa jamii, pia imezingatia kutoa kandarasi mbalimbali kwa wazawa ili kuwajengea uwezo na kuwapa uzoefu wa kupata fursa hata kwa kampuni kubwa mbali na GGML.

Katika kutekeleza malengo ya kanuni  hiyo ya Local Content, zipo changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili kampuni hizo za kizawa kushindwa kufikia vigezo vya ubora na ufanisi wa huduma zinazotakiwa kutolewa kwenye kampuni kubwa za madini kama vile GGML, hivyo katika kuwajengea uwezo wazawa, kampuni hiyo inayofanya shughuli zake za uchimbaji mkoani Geita, imewapa elimu wazawa hao kwa njia mbalimbali ikiwamo semina, warsha na madarasa malumu ambayo yamewawezesha kushinda zabuni na kutoa huduma kwa ufanisi.

Mwanasheria Mwandamizi wa GGML, David Nzaligo anasema juhudi hizo zimewezesha wafanyabiashara wazawa kufaidika na fursa zinazopatikana kwenye sekta hiyo ya madini ikiwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu kwa kuboresha ujuzi wao wa kuandika maandiko ya kibiashara na kushindana ipasavyo katika kuwania fursa zinazopatikana ndani ya GGML.

Kutokana na hali hiyo, idadi ya wafanyabiashara ambao ni wenyeji wa mkoa wa Geita walioingia kandarasi na GGML, imeongezeka kutoka 73 Januari 2020 hadi 96 Desemba 2023, na thamani ya biashara inayotolewa kwa wasambazaji wa Geita imeongezeka kutoka asilimia saba ya matumizi ya ndani mwaka 2020 hadi 9.4 % katika 2023.

Anasema mikakati hiyo ya GGML katika kutekelezwa matakwa ya sheria hiyo ya madini, imekuwa na faida kwa wenyeji wa mkoa wa Geita na hata nje ya mkoa huo.

“Katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 pekee, asilimia 95 ya bajeti ya kampuni ilitengwa kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa makampuni ya Tanzania. Kuongezeka huku kwa manunuzi ya ndani kumesababisha mnyororo wa thamani ya madini kwa jamii inayotunguka kuendelea kuonekana kwa kuwa sasa unastawisha na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wao.

“Kwa mfano, GGML imeingia ubia na wafanyabiashara wa ndani ili kutoa huduma ya usafiri na usambazaji wa mafuta wenye thamani ya zaidi ya Sh 25 bilioni. Mmoja wa waza hao ni kampuni ya Blue Coast Investment Limited inayohusika na usafirishaji wa wafanyakazi ndani ya mgodi na usambazaji wa mafuta. Kampuni hii inafanya kazi za GGML pia nje Geita ikiwamo Dar es Salaam.

“Kampuni nyingine ya ndani ambayo imenufaika kutokana na GGML kutekeleza kikamilifu mikakati ya Local content ni AKO Group. Hii ni kampuni ya kitanzania ambayo imekuwa ikitoa huduma za chakula na usimamizi wa huduma zote za kihoteli ndani GGML tangu 2010,” anasema.

Anasema hatua hiyo inakwenda zaidi ya ushiriki katika shughuli za manunuzi kwani inajumuisha kubadilishana uzoefu na kuwaongezea ujuzi na teknolojia watanzania wanaoshinda zabuni hizo kupitia kampuni zao.

“Nguvukazi ya kampuni ni kipimo cha dhamira hii kwa sababu asilimia 97 ya wafanyakazi wote ni watanzania ambao pia asilimia 80 wapo kwenye timu ya uongozi wa GGML,” anasema.

Awali akizungumza katika kongamano la tatu la ushiriki wa wazawa kwenye mnyororo wa shughuli za madini lililofanyika mkoani Arusha Mei mwaka huu, Nzaligo anasema “Eneo lingine ambalo GGML inatumia kunufaisha wazawa ni pamoja na uhamishaji wa teknolojia na ujuzi. Pia kuwezesha Watanzania kushika nyadhifa ambazo zilikuwa zikishikiliwa na watu wasio Watanzania, jambao ambalo limewezesha vipaji vya ndani kukua na kuwa endelevu kwa GGML,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, GGML imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kukuza na kushirikisha wenyeji katika shughuli za kiuchumi, kubadilisha maisha yao na kuchochea mabadiliko chanya katika shughuli mbalimbali ikiwamo namna ya kupata zabuni kwenye kampuni nyingine nchini.

Kwa kuwa tayari sheria zenye upendeleo kwa Watanzania zipo, muako wa Serikali na kampuni za madini tayari umeonekana dhahiri kuwafungulia milango Watanzania. Huu ndio muda muafaka kwa Watanzania kuguswa na kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye migodi hii kwa sababu manunuzi yaliyofanywa kwenye sekta hiyo katika mwaka wa fedha uliopita ni zaidi ya Sh 3.1 trilioni. Kwa sababu fedha hii ikibaki nchini inatamgusa kila mmoja na hata kubadilisha uchumi wa Taifa  kwa ujumla. Makala hii imeandikwa na Gabriel Mushi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Mpina amng’ang’ania Bashe, kumburuza mahakamani pamoja na bodi ya sukari

Spread the loveMbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) amesema amenuia kumpeleka mahakamani...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Majahazi yadakwa na madumu 1,731 ya mafuta ya kupikia

Spread the loveKikosi kazi cha Polisi Wanamaji Dar es Salaam kimekamata majahazi...

Habari za SiasaKimataifa

30 wafariki dunia maandamano Kenya

Spread the loveShirika la Human Rights Watch limesema takriban watu 30 walifariki...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Tanzania yakubali kukutana na mabalozi 9 kutatua changamoto za kikodi

Spread the loveSerikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na...

error: Content is protected !!