December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jinsi kifo cha kigogo wa Hazina kilivyotokea

Spread the love

JOHANNES Kahangwa (49), aliyefariki 19 Agosti 2019, baada ya kuitumikia Hazina kama Mchumi Mkuu wa Miradi ya Umoja wa Ulaya, amezikwa tarehe 24 Agosti 2018 kijijini kwao Kibona, Kata ya Kanoni, Wilayani Karagwe, Kagera. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mdogo wa marehemu Johannes aitwaye Deusdedith Kahangwa, amemweleza mwandishi wa gazeti hili, kwamba kaka yake (Johannes) alizikwa baada ya ibada ya mazishi iliyoongozwa na Padre Nture, Paroko wa Parokia Katoliki ya Kanoni. 

Akihubiri katika ibada hiyo, Padre Nture aliwasihi waumini kukesha, kuomba na kujitakasa muda wote kwa maana, hakuna mtu yeyote ajuaye siku wala saa ya kuondoka kwake hapa duniani.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na watumishi 15 kutoka Wizara ya Fedha, Makao Makuu Dodoma.

Deusdedith Kahangwa, mdogo wake marehemu akisoma wasifu wa marehemu, aliwaleza waombolezaji kuwa hati ya kifo inaonyesha kuwa Johannes alikufa tarehe 19 Agosti 2019, kutokana na tatizo la kuganda kwa damu (pulmonary embolism) katika mshipa wa moyo uitwao. 

Deusdedith aliwaeleza waombolezaji yafuatayo kuhusu kifo cha kaka yake Johannes:

Kwamba, kabla ya Machi 2019, Johannes hakuwahi kuwa na tatizo lolote la kiafya lililokuwa linamsumbua. 

Ghafla katikati ya Machi 2019 Johannes alipatwa na shambulio kali la kufa ganzi kwa misuli ya mikono, mabega, mapafu, moyo, mbavu za kifua na miguu.

Kati ya Aprili na Juni 2019 Johannes alichukuliwa vipimo mbalimbali ili kubaini chanzo cha shambulio hilo la misuli lakini madaktari hawakuweza kupata jibu lake. 

Vipimo vilifanyika Hospitali ya Agha Khan Dodoma, Appolo Laboratories Dodoma, Hospitali ya Ntyuka Dodoma na Lancert Laboratories ya Moroco Dar es Salaam.

Julai mwanzoni 2019, aliamua kwenda nyumbani Karagwe kuaga familia yake ili arejee Dar es Salaam haraka na kwenda India kwa vipimo vikubwa zaidi.

Agosti mwanzoni 2019, alimfaamisha Deusdedith kuwa tayari ameanza safari ya kurudi Dar es salaam, lakini akasema kuwa anapitia katika Hazina Ndogo Mwanza kwa ajili ya kazi maalum.

Akiwa Mwanza, afya yake iliendelea kuzorota, na kulazwa kwa muda katika Hospitali ya Agha Khan.

Madaktari wa Hospitali ya Agha Khan, Mwanza walimshauri ahamie Hospitali ya Rufaa ya Bugando ili kufanyiwa vipimo maalum walivyoshauri vifanyike. Alipokelewa Bugando tarehe 13 Agosti 2019. Alihudumiwa na kuondoka.

Hata hivyo, hali ilibadilika kwa kasi na hatimaye kupoteza maisha tarehe 19 Agosti 2019 jioni. 

Hayati Johannes Jovin alikuwa Mchumi Mkuu katika Wizara ya Fedha tangu mwaka 2002 mpaka mauti yanamkuta (2019).

Katika kutekeleza majukumu yake, alikuwa msimamizi wa dawati la miradi ya Mataifa ya Umoja wa Ulaya na Marekani, ikiwemo Ujerumani, Ubelgiji, Hispania, Marekani, na Finland. 

Marehemu Johannes alimaliza darasa la saba katika shule ya msingi Kibona Karagwe (1986), kidato cha nne katika shule ya Sekondari Nyakato Bukoba (1990), kidato cha sita katika shule ya Shycom Shinyanga(1993) alikosomea EGM.

Alimaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2000 alikosomea uchumi, na hatimaye mwaka 2007 alipata shahada ya Uzamili (MSc. in Finance) kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, Glasgow, Uingereza. 

Johannes alizaliwa 20 Agosti 1970, akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya Jovin Kahangwa na Matilda Zimbeiya. Ameacha mke na watoto sita.

error: Content is protected !!