July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwandishi wa THRDC aachiwa kwa dhamana Iringa

Joseph Gandye (kulia) akiwa na wakili wake, Chance Luoga muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana

Spread the love

MWANDISHI Joseph Gandye, Mhariri wa Maudhui wa Watetezi TV ameachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi mkoani Iringa, alikokuwa anashikiliwa kwa kosa la kuchapisha habari za uongo mtandaoni. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Gandye ameachwa huru jioni ya leo tarehe 24 Agosti 2019 baada ya kutimiza sharti la kuwa na mdhamini mmoja.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu, Wakili Chance Luoga amesema mwanahabari huyo ametakiwa kuripoti kwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa (RPC), ACP Juma Bwire Jumatatu tarehe 26 Agosti mwaka huu.

“Ameshapata dhamana, baada ya kujitokeza ndugu yake mmoja ambaye ameacha polisi barua ya utambulisho wa serikali ya mtaa anaoishi. Ametakiwa kuripoti kwa RPC Jumatatu saa tatu asubuhi,” amesema Wakili Luoga.

Hata hivyo, Wakili Luoga amesema Gandye hakuhojiwa tena mara ya pili kama alivyoeleza awali Kamanda Bwire, na kwamba hatma yake itafahamika siku ya Jumatatu kama atafikishwa mahakamani au la.

“Jumatatu ndio itajulikana kama atafikishwa mahakamani au hatofikishwa. Tukisharipoti kwa RPC itajulikana nini kinachofuata lakini kwa sasa yuko ameachiwa kwa dhamana,” amesema Wakili Luoga.

Tarehe 22 Agosti 2019 Gandye alipokea wito wa kujisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Urafiki jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, kutoka kwa Askari Polisi aliyejitambulisha kwa jina la Godfrey Mkude.

Baada ya kuhojiwa, Alfajiri ya tarehe 23 Agosti 2019 alisafirishwa na polisi kuelekea mkoani Iringa, mahala anakotuhumiwa kutenda kosa hilo.

error: Content is protected !!