November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JANNY SIKAZWE: Huyu ndiye mwamuzi wa ‘mauzauza’ AFCON 2021

Spread the love

 

Janny Sikazwe ni mwamuzi ambaye ameyatia doa mashinadano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2021) yanayoendelea huko nchini Cameroon baada ya kuitibua timu ya Taifa ya Tunisia kwa kupuliza kipenga cha mwisho kuashiria tamati ya mchezo kati ya timu hiyo na Mali ilihali dakika 90 hazikuwa zimekamlika.

Mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika huibua matukio mbalimbali ya kipekee lakini katika mchezo kati ya Tunisia na Mali almanusura patokee mtifuano.

Benchi la ufundi la Tunisia liliinuka na kwenda kumvaa mwamuzi huyo aliyefanya maamuzi yenye utata kwa kupuliza filimbi mara mbili kuashiria mwisho wa mechi na kukatisha matumaini ya Watunisia kurejesha goli moja walilotunguliwa na Mali katika mchezo huo.

Hata hivyo, baada ya mzozo wa dakika kadhaa timu zote ziliagizwa kurejea uwanjani lakini Tunisia waligoma kufanya hivyo.

JANNY SIKAZWE NI NANI?

MWANAHALISI tunakuletea kila kitu kuhusu tukio hilo la kihistoria.

Janny Sikazwe ni mwamuzi wa soka kutoka nchini Zambia. Sikazwe aliyezaliwa tarehe 26 Mei, 1979, ni mmoja wa waamuzi waandamizi kutoka Zambia akiwa pia ni mwamuzi anayetambulika kimataifa kwa maana Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) tangu mwaka 2007.

Anajivunia uzoefu mkubwa na amechukua jukumu la kuchezesha michezo kadhaa ya hadhi ya juu katika mashindano tofauti, katika ngazi ya vilabu na kimataifa.

Miongoni mwa mashindano ambayo Sikazwe amewahi kuchezesha ni pamoja na Ligi ya Mabingwa wa CAF, Kombe la Dunia kwa upande wa Vilabu na Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia ambayo yote yanaratibiwa na FIFA.

Akiwa mwalimu aliyefunzwa, alipata mafanikio kama mwamuzi mwaka wa 2008 alipochukua nafasi ya mmoja wa waamuzi aliyekuwa mgonjwa kwenye michuano ya CAF ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Tangu wakati huo, kazi yake imekuwa na njia nyeupe kuchezesha mashindano makubwa.

Mwamuzi huyo ndiye aliyechezesha Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015, alichechezesha fainali ya Kombe la Dunia ngazi ya Klabu mwaka 2016 ambapo ilikuwa ni kati ya Real Madrid na Kashima Antlers pia alichezesha fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 kati ya Cameroon na Misri.

Sikazwe ndiye mwamuzi wa kwanza kutoka Zambia kuchezesha mechi katika Kombe la Dunia. Alikamata filimbi katika michezo miwili ya makundi ya Kombe la Dunia 2018 kati ya Ubelgiji dhidi ya Panama na Japan dhidi ya Poland.

Kama wasifu wake unavyooonesha, waamuzi wenzake pamoja na washauri wake wa zamani walimuona kuwa Sikazwe kuwa mwamuzi mwenye viwango kiasi cha kupendekeza kwamba ana uwezo wa kuamuzi wa fainali ya Kombe la Dunia.

“Nilikuwa nikizungumza na Janny kabla hajaondoka kuelekea kwenye Kombe la Dunia – 2018, nikamwambia: “Tayari umefanikiwa kusimamia fainali ya Kombe la Dunia ngazi ya vilabu, hiyo ni hatua ya kuelekea fainali nyingine ya kiwango cha juu FIFA,” Mwalimu wa waamuzi, Felix Tangawarima aliliambia jarida la ESPN la nchini Marekani mwaka 2018.

“Nilimwambia sitashangaa kama atachezesha za fainali ya Kombe la Dunia kutokana na uwezo wake na uzoefu wake mkubwa alioupata CAF. Kila mtu barani Afrika angekuwa na matumaini kwamba anaweza kutuwakilisha katika hatua za mwisho za michuano hiyo.”

Alisimamishwa kwa muda na CAF Novemba mwaka 2018 kutokana na tuhuma za ufisadi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa CAF kati ya Esperance na Primiero Agosto, hata hivyo adhabu hiyo iliondolewa Januari 2019 katika kikao cha kinidhamu kilichoketi.

NINI KILITOKEA TUNISIA DHIDI YA MALI AFCON 2021?

Mzozo ulianza katika wa mchezo kati ya Tunisia na Mali kwenye mashindano hayo ya Afcon 2021 tarehe 12 Januari, 2022 baada ya Sikazwe kupiliza kipenga cha kuashiria kumaliza mchezo huo kwa nyakati mbili tofauti.

Awali alipuliza kwamba muda umeisha lakini ilikuwa dakika 85, dakika tano kabla ya muda wa kanuni za mecho wa soka.

Kisha mara nyingine tena kabla ya dakika 90 kuhitimu alipuliza kipenga na kusababisha mtafaruku katika benchi la timu ya taifa ya Tunisia, ambayo ilikuwa nyuma kwa 1-0.

Hali hiyo iliibua mkanganyiko mkubwa baada ya kumalizika kwa mchezo huo, huku mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi ukikatizwa baada ya CAF kuamuru timu zote kurejea mchezoni huku mwamuzi akibadilishwa kwa dakika tatu za mwisho.

Wakati wachezaji wa Mali wakirejea uwanjani, Tunisia walichagua kumpinga na matokeo yakabakia kuwa Mal I kuondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya waarabu hao.

Makala hii imeandaliwa na Gabriel Mushi.

error: Content is protected !!