December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jaji Warioba avinyooshea kidole vyombo vya habari  

Jaji Joseph Warioba

Spread the love

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Joseph Warioba, amekosoa utendaji wa vyombo vya habari nchini humo akisema vinasuasua kutoa habari zinazohusu masuala ya wananchi na kujikita kutoa habari zinazohusu uongozi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Warioba aliyekuwa waziri mkuu kuanzia 5 Novemba 1985 hadi 9 Novemba 1990 katika utawala wa awamu ya pili ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema hayo jana Ijumaa tarehe 20 Novemba 2020 wakati akizindua Bodi mpya ya Baraza la Habari Tanzania (MCL).

Akitumia takribani dakika zisizozidi 20, Warioba alieleza mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii na nchi na jinsi ulivyomsaidia kushughulikia matatizo mbalimbali akiwa waziri mkuu.

Warioba aliyewahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki alisema, ingawa kwa sasa Tanzania kuna vyombo vingi vya habari ikilinganishwa na miaka ya nyuma,  lakini vinashindwa kuweka usawa katika utoaji habari za uongozi na wananchi.

Alisema, miaka ya nyuma wananchi walikuwa wanapata nafasi za kutosha kutoa ama kufikisha maoni yao kwa viongozi kupitia vyombo vya habari, lakini kwa sasa nafasi hizo hakuna za kutosha.

“Redio Tanzania ya wakati ule ilikua inatoa habari za wananchi na wananchi walikuwa na nafasi kupeleka maoni yao, kuna kipindi kimoja walikuwa wanakwenda kijiji kuchukua habari za wananchi.”

“Ila vyombo vya habari vya sasa, havielezi wananchi wanafanya nini wanatoa habari za uongozi,” alisema Warioba aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Jaji Juxon Isaac Mlay, Rais wa Bodi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT)

Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema, hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kukosa imani na vyombo vya habari vya Tanzania badala yake vinasikiliza vyombo vya habari vya nje akitolea mfano BBC, CNN, DW au VoA.

“Kwa sasa mtu akimuuma mbwa sio habari, tunataka habari za mbwa ana muuma mtu,  kama ‘media’ inaogopa kusema mtu ameuma mbwa matokeo yake ni nini, matokeo yake watu sasa wanaanza kuona kama ni jambo la kawaida kusikiliza habari kutoka nje,” alisema Jaji Warioba.

Warioba aliyezaliwa tarehe 3 Septemba 1940, Bunda mkoani Mara alisema, kitendo cha vyombo vya habari kutotekeleza wajibu wake ipasavyo, kunasababisha viongozi kukosa maoni, ushauri na elimu kutoka kwa wananchi.

“Ikija suala Fulani, unasikia wananchi wapewe elimu lakini tuna sahau uongozi lazima upate elimu kutoka kwa wananchi na lazima maoni ya wananchi yatoke katika vyombo vya habari,” alisema Jaji Warioba.

Akirejea utendaji wa vyombo vya habari katika miaka iliyopita, Jaji Warioba alisema, vilijitahidi kuchimbua habari zinazohusu masuala ya wananchi.

“Wakati nchi ilikua inaingia kwenye mfumo wa siasa wa vyama vingi, habari zilikua nyingi na tunaendelea hivyo hivyo. Ila sasa sina hakika, lazima niseme kama vyombo vya habari imekomaa kiasi cha kutosha  kutoa habari za kila aina kwa wananchi.”

“Wakati yulipokuwa chini ya mfumo wa chama kimoja, vyombo vya habari vya Serikali,  wakati ule kulikuwa na malalamiko habari hazitoki lakini zilikua zinatoka,” alisema Jaji Warioba.

Akielezea historia ya uongozi wake akiwa waziri mkuu, Warioba alisema  vyombo vya habari  vilimsaidia kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.

Alisema, alipokuwa waziri mkuu alikuwa anapata maoni na changamoto za wananchi kupitia vyombo vya habari hasa magazeti.

Jaji Warioba alisema, katika ofisi yake kulikuwa na mtu maalum aliyekuwa anamkusanyia habari na maoni ya wananchi yaliyochapishwa katika magazeti.

“Wakati ule magazeti yalikuwa na nafasi ya maoni ya wananchi. Nilipo kuwa waziri mkuu, nilikuwa na msaidizi wa mambo ya habari, alinisaidia sana kila asubuhi nikienda ofisini nakuta lundo la gazeti.”

“Alikua anatia alama sehemu za kusoma,  alikua ananionesha kipi nisome nipate kujua hali ikoje nchini na duniani,” alisema Jaji Warioba.

“Pili, alikuwa anaweka alama katika tahariri ambazo anaona ni muhimu nisome, lakini sehemu kubwa alikua ana weka alama maoni ya wananchi.  Sina hakika kama vyombo vya habari za kwetu zina nafasi za kutosha kuleta maoni ya wananchi.”

Jaji Warioba amevishauri vyombo vya habari kutimiza majukumu yao kikamilifu kwa kuzingatia usawa katika utoaji habari, ili wananchi warudishe imani yao kwa vyombo vya habari  vya ndani.

“Mimi nina tabia kama niko kwenye gari inafika wakati saa ambayo najua kuna habari napenda kusikiliza habari, kwa hiyo madereva wangu walizoea ikifika saa saba wananifungulia redio one au TBC kusikiliza habari.”

“Polepole nilianza kuona mabadiliko ikifika saa saba nafunguliwa D.W, kumbe hata watu wa kawaida wanajua ‘station’ za nje,” alisema Jaji Warioba ambaye sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.

Bodi iliyozinduliwa

Bodi iliyozinduliwa, inaongozwa na Rais, Jaji Juxon Isaac Mlay na Makamu wake, Yussuf Yussuf ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar (Zanzibar Leo)

Pia, Yussuf atakuwa mkuu wa Kamati ya fedha na utawala.

Wengine katika kamati hiyo ni; Tido Mhando ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Happiness Nkya atakayekuwa Kamati ya ukaguzi wa mahesabu  ya baraza, Dk. Joyce Bazira, Teddy Mapunda, Bakari Machumu, Edda Sanga na Anna Henga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

error: Content is protected !!