Tuesday , 16 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Halima Mdee, wenzake hawachomoki
Habari Mchanganyiko

Halima Mdee, wenzake hawachomoki

Spread the love

HALIMA James Mdee, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), “amenasa kwenye ndoana.” Hawezi tena kuchomoka. Anaripoti Mwandishi Maalum…(endelea).

Pamoja na kelele za tarumbeta zilizopigwa kumjulisha hatari ya anguko lililokuwa linamkabili, bado aliendelea kutetea alichokifanya.

Miaka takribani 15 ya Mdee ndani ya Chadema na kwenye mageuzi nchini, inakwenda kukatika kesho Ijumaa.

Anguko la Mdee kisiasa, linakuja mwezi mmoja baada ya kumalizika uchaguzi mkuu. Alikuwa mmoja wa wabunge mahiri wa Chadema, katika Bunge lililopita na katika uchaguzi mkuu wa majuzi, alijitosa kutetea tena kiti chake cha ubunge jimbo la Kawe.

Amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 10 mfululizo na amekuwa bungeni, tokea mwaka 2005, ambapo alianzia kwenye Viti Maalum.

Ndani ya kipindi hicho, Mdee amepitia dhoruba mbalimbali, ikiwamo kuhukumiwa kifungo au faini; kusimamishwa kuhudhuria mikutano ya Bunge, kushitakiwa Kamati ya Maadili ya Bunge na mahakamani na kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara jimboni kwake.

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Mpaka sasa, Mdee bado anakabiliwa na kesi nyingine kadhaa za jinai, mahakamani na polisi.

Kamati Kuu (CC) ya Chadema, inatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam, kesho Ijumaa, tarehe 27 Novemba 2020, kujadili sakata la Mdee na wenzake 18, walioapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri, bila ridhaa ya chama hicho.

Jumanne iliyopita, Mdee na wanachama wenzake hao, waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge wa Bunge la 12 Tanzania, kinyume na msimamo wa chama chao ambacho kinachoamini kitendo hicho, kinahalalisha uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba 2020.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, alitangazwa mshindi wa kiti cha urais, huku Chadema, kikiambulia kiti kimoja cha ubunge jimbo la Nkasi Kaskazini.

Wanachama hao walioapishwa kuwa wabunge, ni pamoja na Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega;  Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Ester Bulaya; Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta  Lambat; Makamu Mwenyekiti, Hawa Subira Mwaifunga; Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Serengeti, Esther  Matiko na Naibu Katibu Mkuu  Bawacha (Bara), Jesca Kishoa.

Wengine, ni Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje; Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara,  Tunza Malapo; aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum, mkoani Arusha, Cecilia Pareso na aliyekuwa mbunge wa mkoani Mbeya na katibu msaidizi wa wabunge wa Chadema, Sophia Mwakagenda.

Wapo pia, aliyekuwa mbunge wa Same Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka na waliokuwa wabunge wa Viti Maalum, Kunti Majala (Dodoma);  Anatropia Theonest (Dar es Salaam), Salome Makamba (Shinyanga), Conchesta Lwamlaza (Kagera), Stella Siyao, Asia Mwadin Mohamed na Felister  Njau.

Swali la kujiuliza ni hili: Mdee amefikishwaje kwenye kitanzi hiki? Nani aliyemuingiza mkenge mwanasiasa huyu shupavu? Kipi kilichomsukuma kuchukua maamuzi haya magumu, wakati anajua kuwa taratibu, kanuni, katiba na miiko ya chama chake, haviruhusu jambo hilo? Tujadili:

Mdee ndiye mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha). Katika sakata hili, anatajwa kuwa kinara wa mpango mzima wa “usaliti ndani ya chama chake.”

Kwa mujibu wa taarifa ndani ya Chadema, Mdee alishirikiana na Tendega, Bulaya, Agnesta na Kunti, kupeleka majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Bunge, ili hatimaye waweze kuteuliwa na kuapishwa kuwa wabunge.

Katika kutekeleza kazi hiyo chafu, Mdee aliongea na baadhi ya viongozi wandamizi wa CCM, Bunge, NEC na hata baadhi ya watu walioko “kwenye mfumo,” ili kufanikisha kile ambacho anadai ni haki ya wanawake wa Chadema.

Madai haya yanathibitishwa na hatua ya Spika Job Ndugai, kuwaapisha katika kipindi ambacho hakukuwa na mkutano wa Bunge.

Katika historia ya Bunge la Tanzania, hii ilikuwa mara ya kwanza kwa kundi kubwa la wabunge wa upinzani kuapishwa kwa wakati mmoja wakati hakuna mkutano wa Bunge unaoendelea.

Kwa kawaida, wabunge wamekuwa wakiapishwa wakati kuna mkutano wa Bunge. Ndio maana Spika Ndugai amelazimika kujaribu kutetea hilo kwa kusema, “kanuni zinataka wabunge waapishwe mbele ya Spika na si lazima iwe wakati wa vikao vya Bunge.”

Aidha, madai haya yanapata nguvu zaidi, kutokana na kitendo cha serikali kumuachia huru Nusrat kutoka gerezani alikokuwa akishikiliwa tokea Julai mwaka huu, usiku na siku iliyofuata – tarehe 24 Novemba, kuapishwa kuwa mbunge.

Nusrat na wenzake, waliachiwa huru na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa kile alichoita, “Jamhuri haina tena nia ya kuendelea na kesi hiyo,” bila kufikishwa mahakamani.  Mdee anajua yote haya.

Anajua Nusrat hakushiriki mchakato wa ndani ya Chadema katika kuwatafuta wabunge wa viti maalum. Anajua wakati mchakato unaendelea, Nusrat alikuwa mahabusu mkoani Singida.

Si hivyo tu: Mdee na wenzake wameapishwa kuwa wabunge, bila kujaza fomu Na. 8(d) wanayopaswa kujaza wabunge wa Viti Maalumu.

Kifungu C katika fomu hiyo, kinataka kuwapo uthibitisho wa vyama kutoka kwa katibu mkuu au naibu wake, pamoja na mhuri wa chama husika.

Mdee na wenzake, hawakujaza fomu hiyo, hawakugonga mhuri, wala hawakwenda mahakamani kula kiapo, wakati wanajua kuwa hayo ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kufanyika kwa mtu anayetaka kuwa mbunge kwa mujibu wa sheria.

Katika mazingira haya, hakuna namna ambako unaweza kusema, mchakato huu wa kutafuta wabunge wa Viti Maalum wa Chadema, haukuingiliwa na watu waliko nje ya chama hicho.

Au hakuna namna ambayo unaweza kusema, Mdee hakushiriki au kushirikiana na watu ambao siyo wanachama wa Chadema, kukiteulia chama hicho wabunge wake.

Hakuna namna ya kuweza kumtetea Mdee, kuwa hakusaliti chama chake katika jambo hili. Hakuna namna ambayo Mdee anaweza kueleza na akaeleweka, kwamba kwa nini aliamua kutafuta usaidizi wote huu nje ya chama, badala ya kushawishi wenzake ndani ya chama. Hakuna.

Katika muktadha huo, Chadema ina njia moja tu iliyosalia. Ni kumfukuza Mdee na wenzake wote ndani ya chama chao. Hiyo angalau yaweza kusaidia kurejesha hadhi na heshima ya chama hicho, mbele ya jamii. Yaweza kusaidia kurejesha ari ya wanachama kwa chama chao.

Nje ya hapo, Chadema na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ambaye ametajwa na Mdee kuwa “mshirika wa jambo hili,” watakuwa wanakichimbia kaburi chama hicho kwa mikono yao wenyewe.

Hii ni kutokana na  ukweli kwamba, tukio hili siyo la kwanza kutokea ndani ya Chadema. Miaka mitano iliyopita, chama hiki kiliwavua uwanachama, madiwani wake sita – watano wa kata na mmoja wa viti maalum – katika jiji la Arusha.

Chadema iliwafukuza pia waliokuwa wabunge wake, David Silinde, Anthony Komu na Willifred Muganyizi Lwakatare, wiki moja kabla ya kumalizika Bunge la 11 kwa madai walikwenda kinyume na maelekezo ya chama ya kutoingia bungeni, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Corona.

Mdee ameshiriki katika vikao vilivyofanya maamuzi yote haya na mengine yanayofanana na hayo. Anajua kuwa anachokifanya ni kosa. Lakini aliamua kufanya. Ni kwa sababu, ameshaamua liwalo na liwe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Sekta binafsi yasifu utekelezaji wa Mkumbi

Spread the loveSERIKAL imepongezwa kwa utekelezaji wa mapendekezo ya sekta binafsi kupitia...

Habari Mchanganyiko

Kamati ya bunge yapigia chapuo kilimo ikolojia

Spread the loveSERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeshauriwa kushirikiana na wadau wa...

Habari Mchanganyiko

Serikali yapata hasara 113 milioni hospitali kuwapa misamaha wagonjwa wasiostahili

Spread the loveSERIKALI imepata hasara ya kiasi cha Sh. 111.76 milioni, baada...

Habari MchanganyikoMichezo

NBC, Yanga wazindua kadi  za kimataifa za uanachama

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Klabu...

error: Content is protected !!