WANANCHI wa Materereka katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, mkoani Ruvuma wamesema ujenzi wa kituo cha afya kilichojengwa kwa fedha za tozo za miamala umekuwa kama ndoto kwao kwa sababu hawakutarajia kusogezewa karibu huduma za matibabu. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Wananchi walieleza hayo juzi mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri ya Madaba, Sajidu Mohamed aliyefanya ziara ya kukagua mwenendo wa ujenzi wa kituo hicho kilichogharimu Sh milioni 250.
Kituo hicho kimejengwa katika eneo ambalo litasaidia asilimia kubwa ya wananchi kupata huduma za matibabu kwa urahisi bila kulazimika kwenda maeneo mengine ya jirani.
Mmoja wa wananchi hao, Constatine Mlelwa amesema wanaona kama ndoto kwa namna walivyokuwa wakihangaika kupata huduma za matibabu, wakilazimika kutumia gharama kubwa kwenda hospitali ya wilaya ya Madaba au mkoani.
“Kwa niaba ya wananchi wa Matetereka tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutujengea kituo cha afya hapa. Kituo hiki kitatumika na wananchi wa vijiji vya Maweso, Matetereka na Mwande kwa sababu hata upasuaji utafanyika hapa,” alisema Mlelwa.
Naye Deograsius Mponda anayeishi Matetereka akiwa na watoto saba, amemshukuru Rais Samia kwa kuwaona kwa jicho la huruma kwa kuwasogezea huduma za matibabu kwa ngazi ya kituo cha afya akisema wamekuwa wakipata adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta matibabu.
“Nina watoto saba lakini natamani nizae mtoto mwingine katika kituo hiki cha jirani maana kipo karibu na makazi yangu. Mungu ambariki Rais Samia kwa moyo wake wa upendo wa kuwajali wananchi mbalimbali hasa wa vijijini.
Kwa upande wake, Rogatha Matei mkazi wa kijiji cha Mwande amesema huduma za afya wanapata katika zahanati ya Matetereka lakini wakihitaji matibabu makubwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 20 hadi Madaba.
“Umbali wake ukipanda pikipiki Sh 1,000 hadi halmashauri, tulikuwa changamoto kubwa hasa wajawazito ambapo kama huna fedha huwezi kufika Madaba. Lakini kituo hiki kikikamilika kitakuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Matetereka.
Akizungumzia ujenzi huo, Mkurugenzi Mtendaji, Mohamed amesema ujenzi huo unakaribia kukamilika na kituo hicho kikianza kutoa huduma kitakuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Materereka ambao kwa nyakati tofauti walilazimika kufuata huduma ya matibabu huko Madaba.
Leave a comment