February 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Familia yaelezea ushujaa halisi wa Ruge  

Mwachi Mutahaba akisoma wasifu wa baba yake, Marehemu Ruge Mutahaba

Spread the love

WASIFU uliosomwa na Mwachi Mutahaba ambaye ni mtoto wa kwanza wa Ruge Mutahabu, mwanahabari aliyekuwa mtayarishaji wa vipindi vya Clouds Media Group (CMG), umeibua taswira halisi ya wanaharakati huyo wa maendeleo nchini. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Ikiwa wengi wakimfahamu Ruge kwa kiasi kidogo, wasifu wake uliosomwa na kijana huyo (Mwachi) kwa niaba ya familia mbele ya umati wa watu waliofurika kumuaga katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam leo tarehe 2 Machi 2019, umefunua yaliyokuwa yamefunikwa.

Mwachi anasema, matokeo ya namna alivyokuwa Ruge katika maisha kabla ya kifo chake, yanaakisi alikopita na kazi alizokuwa akizifanya kwa kuwa, hakukata tamaa.

Amesema, enzi za uhai wa Ruge, alipenda kujihusisha na tasnia ya burudani hususan muziki na kwamba, aliwahi kufungua kampuni ya kutengeneza video pamoja na kuandaa matamasha mbalimbali ya sanaa kuanzia ngazi ya nyumba 10 na kuendelea.

“Damu ya Ruge ilikua kwenye muziki na hapo ndipo aliposhikilia, alianza mapema kupenda muziki, lakini alifanya mambo makubwa sana.

“Ujasiriamali wa Ruge ulianza mbali sana, aliandaa event (tukio) ya nyumba 10 ilikuwa uimbaji, sarakasi na maigizo ya nyumba 10, tiketi ilikuwa Sh. 10. Waliokuwa wakishiriki walikuwa wakifurahi,” amesema Mwachi na kuongeza;

“Hii damu ya muziki na ujasiriamali iliendelea kukaa pale pale, Ruge na Uncle Joseph (mjomba) walianzisha kampuni yao ya video na wakawa wanafanya tafrija wakati wakiwa bado wanafunzi wa ssekondari.”

Historia hii inaungana na ile aliyoitoa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete aliposema alimfahamu Ruhe katika masuala ya burudani na matamasha kwa miaka 20 iliyopita.

Akizungumzia mapito ya elimu yake Mwachi amesema, Ruge alizaliwa tarehe 1 Mei 1970 jijini New York, Marekani na kuwa mtoto wa kwanza kati ya watoto watano wa Prof. Gerald Mutahaba na Christina Mutahaba.

Amesema, Ruge alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Arusha hadi Darasa la VI na kuhamia Shule ya Msingi Mlimani alikohitimu elimu ya msingi, kisha akaendelea na Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Forodhani.

Baada ya kuhitimu Elimu ya Sekondari aliendelea na masomo ya Kidato cha V na VI katika Shule ya Sekondari Pugu. Alihitimu Shahada ya Masoko na Shahada ya Sanaa katika Uchumi kwenye Chuo Kikuu cha San Jose huko California, Marekani.

Kwenye shughuli ya kuuaga mwili wa baba yake Mwachi amesema kwamba, familia yao inatambua kuwa Ruge alikuwa ni mfanyabiashara, na kwa namna moja au nyingine anaweza kuwa amewakosea watu, hivyo familia inamwombe wamsamehe ndugu yao aende kwa usalama, na pia wao kama familia wamewasamehe wale waliomkosea.

“Kama binadamu tunatambua kuna wale aliowakwaza kwa namna moja au nyingine, kwa niaba ya familia tunaomba mumsamehe, na sisi kama familia tunawasamehe wale ambao kwa namna moja au nyingine walimkosea,” amesema Mwachi.

Mwili wa Ruge ueagwa leo katika uwanja wa Karimjee ambapo vviongozi wakuu wa serikali wakihudhuria akiwemo Rais John Magufuli; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na viongozi wengine wa serikali na kisiasa.

Ruge ameacha watoto watano, wazazi wake na wadogo zake wanne. Mwili wake unatarajiwa kusafirishwa kesho tarehe 3 Machi 2019 kwenda Bukoba mkoani Kagera kwa mazishi yatakayofanyika Jumatatu tarehe 4 Machi 2019.

error: Content is protected !!