Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF:  Tupo tayari kushirikiana lakini… 
Habari za SiasaTangulizi

CUF:  Tupo tayari kushirikiana lakini… 

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania,  kimetoa msimamo kuwa kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya upinzani vyenye dhamira ya kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo tarehe 6 Juni 2020, na Juma Killghai, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, alipokuwa akitoa ratiba ya kuwapigia kura za maoni na uteuzi watia nia wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu 2020.

Killghai amesema, chama hicho kitashirikiana na chama chochote chenye dhamira ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani.

“…chama chetu kipo tayari kushirikiana na chama chochote chenye dhamira ya kweli ya kuiondoa CCM na kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi, isiwe kinaingia madarakani kinafanya yaleyale yaliyokuwa yakifanya na CCM,” amesema

Amesema, mchakato wa kugawana majimbo ama kata utafanyika kwa utaratibu watakaokubaliana baina yao na chama ambacho kitaafikiana nacho.

Akiizungumzia ratiba ya kura za maoni na uteuzi ndani ya chama hicho, amesema uandaaji wa fomu za utiaji nia umeanza tangu tarehe 5 Mei 2020 na kwamba urejeshaji wa fomu utahitimishwa tarehe 27 Julai 2020.

Amesema chama hicho kimejidhatiti kusimamisha wagombea wa nafasi zote nchi nzima na kuwataka wanachama wote wenye sifa kujitokeza kugombea.

“Tunatarajia kuweka wagombea nchi nzima katika ngazi za udiwani, uwakilishi na ubunge.”

“Aidha, tunatarajia kusimamisha wagombea Urais wawili, mmoja akisimama kwa ajili ya Urais wa Zanzibar na mwingine akisimama kwa ajili ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Killghai ametumia fursa hiyo, kuwataka wanachama wa chama hicho wenye sifa, kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za kukiwakilisha chama katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

“Tunapenda kuwahakikishia chama hakina wagombea “wateule.” Kila mwanachama mwenye sifa, atapewa nafasi sawa na mwingine na matakwa ya wajumbe watakaoshiriki kupiga kura za maoni ndiyo ambayo yatapewa kipaumbele labda itokee kwamba kuna sababu za msingi za kutengua maambuzi hayo,” amesema

Kauli ya CUF kuhusu kushirikiana, wameitoa ikiwa zimepita takribani siku nne tangu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufungua milango ya majadiliano na vyama vingine vya siasa ambavyo vinadhamira ya kweli ya kushirikiana kuiondoa CCM madarakani.

Jumatano iliyopita ya tarehe 3 Juni 2020, Katibu Mkuu wa Chadena, John Mnyika akizungumza na wanadishi wa habari alisema, “Tunafungua mlango wa majadiliano na vyama ambavyo vinadhamira ya kweli ya kushirikiana kuiondoa CCM madarakani.”

Katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, CUF na Chadema vilikuwa miongoni mwa vyama vine vilivyoshirikiana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Vyama vingine vilikuwa NLD na NCCR-Mageuzi. Katika ushirikiano huo, walisimamia mgombea mmoja mmoja kwa udiwani ubunge na urais wa pande zote wa Tanzania na Zanzibar.

Ukawa ulioanzia Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014 umekuwa ‘upo au haupo’ kutokana na washirika wa vyama hivyo, kila mmoja kuendelea kivyake.

CUF ilitengwa na Ukawa mara baada ya Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wake, kutangaza kujizulu katikati ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kisha baadaye kurejea kwenye nafasi hiyo, hali iliyoibua mvutano mkali.

Mvutano huo, ulifika mahakamani na Mahakama kutambua uenyekiti wake jambo lililomfanya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wenzake waandamizi hususan upande wa Zanzibar kutimkia ACT-Wazalendo.

Kwa sasa Maalim Seif ni Mweneykiti wa ACT-Wazalendo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!