May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

COVID-19: Sheikh Ponda aungana na KKKT, Katoliki

Sheikh Issa Ponda, Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu

Spread the love

SHEIKH Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, amepongeza miongozo iliyotolewa na Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjiki la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuhusu kujilinda na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza na Mwanahalisi Online leo tarehe 14 Februari 2021 amesema, miongozo hiyo imewazindua waumini wao kuonesha kuna tatizo na hatua za haraka zinahitajika.

“Wito uliotolewa na makanisa hayo, si kwa waumini wao tu bali ni wito kwa Watanzania wote.

“Naamini kila Mtanzania sasa anajua tatizo lipo, kila mmoja ana jukumu la kujilinda yeye mwenyewe na watu wake. Anayedhani uhai wake uko mikononi mwa dola, asaidiwe,” amesema Sheikh Ponda.

Hivi karibuni viongozi wa makanisa hayo, walitoa miongozo kwa waumini wao wakiwataka kufuata kanuni ili kujilinda na maambukizi ya virusi ikiwemo corona.

Amesema, kuna mkanganyiko kuhusu taarifa za corona nchini, na kwamba jambo hilo linawaweka wananchi njia panda.

Akizungumzia kauli ya Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbas kwamba corona imeangamizwa nchini, amesema hajajua silaha gani zimetumika kumaliza tatizo hilo.

“Ninachojua ni serikali ilisitiza utoaji taarifa basi, ilifanywa upuliziaji dawa mara tukaambiwa inaua mende tu, hizo njia za kisayansi zilizoelezwa mimi sikuziona.

“Nadhani hakuna haja ya kutaka kuelezwa na mamlaka yoyote kuhusu janga hili, kila mmoja anapaswa kuchukua hatua,” amesema.

Amesema, taasisi yao bado inasimamia miongozo waliyoitoa mwaka jana kuhusu kujilinda dhidi ya magonjwa hayo.

“Inapendeza misikitini kwetu kila muumini kabla ya kugungua bomba, anapaswa kuwa na sabuni mkononi kisha ndio anawe kabla ya kuchukua udhu.

“Tusijidanganye kwamba hakuna tatizo, umakini uwepo na kazi ziendelee kwa tahadhari ile ile,” amesema Sheikh Ponda.

error: Content is protected !!