CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kumuunga mkono Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na kuachiana majimbo na kata na chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumapili tarehe 4 Oktoba 2020 na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema wakati anatangaza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho, iliyoketi jana Jumamosi jijini Dar es Salaam.

Mbowe amesema, uamuzi huo umekuja baada ya Mgombea Urais wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohammed kuridhia kujitoa katika kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono Maalim Seif.
“Sisi kama Kamati Kuu jana tumeamua na kuridhika na kauli za viongozi wa vyama vyetu hususan Chadema na ACT baada ya kushauriana kwa kina na mgombea wetu wa Zanzibar tumeona ni sahihi chama chetu kumuunga mkono Maalim Seif na kwa maana hiyo anaridhia kujitoa kwa hiari yake,” amesema Mbowe
Mbowe amesema, Kamati Kuu za Chadema na ACT-Wazalendo ziko katika utaratibu wa kutafuta namna watakavyoshirikiana katika Uchaguzi wa wabunge na madiwani kwa pande zote mbili, Tanzania Bara na Zanzibar.
“Chama chetu kimeona umuhimu wa ushirikishwaji wa ngazi mbalimbali za chama katika kuungana kwenye kusimamisha wagombea wa ubunge na udiwani, tumeziachia kamati (za Chadema na ACT-Wazalendo) kufanya mazungumzo kwa haraka kuona tunaachianaje majimbo na kata,” amesema Mbowe.
Leave a comment