October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CCM kumweka kikaangoni Mwita Waitara

Mwita Waitara

Spread the love

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Mara kimesema kitamuita kwenye Kamati ya Maadili, Mwita Waitara, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ili kujibu tuhuma za kuvunja kanuni za uchaguzi za chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Akizungumza na Wanahabari jana tarehe 3 Januari 2020, Samweli Kiboye, Mwenyekiti wa CCM Mkoani Mara, amesema Waitara amefanya makosa kujinadi kuwa atagombea Jimbo la Tarime Vijijini,  kinyume na katiba ya chama hicho, kwa kuwa kipindi cha uchaguzi bado hakijafika.

“Lazima tutumie kanuni zetu za CCM,  kanuni za uchaguzi, lazima tumwite katika vikao vyetu hatuwezi kumuacha mtu anajinadi. Kwa sababu akishaanza kujinadi ataleta makundi Tarime, tunataka WanaTarime tuikomboe Tarime, tunavyoenda hivi tutaleta makundi,” amesema Kiboye.

Mwenyekiti huyo wa CCM mkoani Mara, amesema Mwita ataitwa kwenye kamati hiyo, ili kujibu utaratibu aliotumia kujitangaza kugombea Ubunge wa Tarime Vijijini.

“Atatueleza ametoa mfumo wake wapi wa kujitangaza, au kama yeye anajiona yuko juu ya chama ndani ya Tarime, asije akatuharibia chama Wilaya ya Tarime,” ameeleza Kiboye.

Kiboye ameonya watu wanaoanza kujinadi kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, akisema kwamba, hatamuogopa mtu yeyote kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya CCM.

“Natoa onyo vikao vitafuata na hatutamuonea mtu haya, hatutamuogopa yeyote awe na cheo kiasi gani, chama ndio kikubwa. Hakuna mtu aliyejuu ya chama, chama ndio bosi uhoji mtu yeyote, lazima tuwahoji tutawaita katika kamati ya maadili,” ameonya Kiboye.

Mwita ambaye ni Mbunge wa Ukonga, hivi karibuni alitangaza kugombea ubunge wa jimbo hilo, na kuahidi kuchuana na John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

error: Content is protected !!