April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kusimamishwa wanafunzi UDSM: BAVICHA kuiburuza Serikali mahakamani

Spread the love

BARAZA la Vijana la Chama cha Chadema (BAVICHA) limesema litafungua kesi mahakamani, ili kupinga hatua ya Uongozi wa Chuo cha Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana, wanafunzi wa chuo hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Mnamo mwezi Desemba 2019, uongozi wa chuo hicho uliwasimisha masomo wanafunzi sita, akiwemo Hamis Mussa, Rais wa Serikali ya Wanafunzi UDSM (DARUSO).

Ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, baada ya wanafunzi hao kutoa tamko la kuitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),  kutatua changamoto ya fedha za mikopo,  ndani ya saa 72.

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 4 Januari 2020, John Pambalu, Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, amesema watakwenda Mahakamani ikiwa, Kamati ya Maadili ya chuo hicho, haitawatendea haki wanafunzi hao.

“Kwa sasa kuna taratibu zinazosubiriwa,  ikiwemo kusubiri kamati ya maadili ya chuo hicho kufanya maamuzi yao. Ikiwa kamati ya maadili ya chuo italinda haki yao, hatutakwenda mahakamani lakini kamati ya maadili ya chuo isipotaka kutoa haki tutaenda mahakamani,” ameahidi Pambalu.

Aidha, Pambalu ameitaka serikali kuweka wazi kama haiwezi kutoa fedha za mikopo kwa wanafunzi, kama ilivyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Serikali itoke nje iwaambie kwamba suala la mikopo haiwezi kutekelezeka. Tuko tayari kusimama na vijana wenzetu walio ondolewa UDSM. Tuko tayari kwenda mahakamani kutetea vijana ili wapate elimu,” amesema Pambalu.

Wanafunzi hao walisimamishwa masomo kwa muda usiojulikana, baada ya kutoa tamko la saa 72,  kutatua changamoto ya utolewaji wa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa UDSM, ikiwemo waliocheleweshewa fedha hizo, na wale waliokatwa fedha kutokana na sababu mbalimbali.

 

 

error: Content is protected !!