December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Bwege alazwa Muhimbili

Suleiman Bungara 'Bwege'

Spread the love

 

ALIYEKUWA Mbunge wa Kilwa Kusini mkoani Lindi, Said Bungara ‘Bwege’, amelazwa katika wodi ya Sewahaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akiugua kwa muda mrefu uvimbe kwenye shavu la kulia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Bwege alikuwa Mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), kwa takribani miaka 10 ambapo uwakilishi wake ulivutia watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Mwaka 2020 aligombea kupitia ACT-Wazalendo na kushindwa.

Akizungumza na MwanaHALISI Online Bwege amesema amekuwa akisumbuliwa na uvimbe huo ulitokea kwenye shavu la kulia kwa muda mrefu, hali iliyomsababishia maumivu makali.

Bwege amesema uvimbe huo ulikuwa unamletea dalili za kupooza, hivyo ikamlazimu kwenda Hospitali ya Muhimbili kufanya uchunguzi na wiki iliyopita alifanyiwa upasuaji na madaktari bingwa wa hospitali hiyo.

Alishukuru madaktari waliomfanyia upasuaji huo, ambao ulikwenda vizuri na kwamba ni matumaini yake atatoka mapema.

“Ni kweli nimelazwa hapa Muhimbili na juzi nilifanyiwa upasuaji ambao ulikwenda salama na kwa sasa nadiriki kusema naendelea vizuri, Mungu akipenda nitatoka madaktari wakiamua,” amesema.

Mbunge huyo wa zamani ambaye amejitengenezea umaarufu kwa kupigania haki za wapiga kura wake, amesema tangu afanyiwe upasuaji anaendelea vizuri.

Aidha, Bwege ambaye amekuwa maarufu kutokana na misemo yake iliyojaa vichekesho, alisema tofauti na changamoto hiyo aliyokutana nayo, pia anasumbuliwa na kisukari.

Bwege ameomba wananchi wamwombee ili afya yake iweze kutengamaa na aweze kuendelea kupigania nchi kama kawaida yake.

“Nimekuwa nikifanya kazi ya siasa kila siku na tatizo hili nilikuwa nalo, lakini baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, nimekuja Muhimbili, nashukuru kuwa dalili za kuendelea kujenga nchi kupitia siasa zitaendelea,” amesema.

error: Content is protected !!