Mkutano wa 14 wa Bunge la 12 uliopangwa kufanyika kwa muda wa wiki tatu kuanzia kesho tarehe 30 Januari hadi tarehe 16 Februari 2024 unatarajiwa kuanza kujadili miswada mitatu iliyowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba mwaka jana. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Miswada hiyo ambayo imeibua mjadala pamoja na kupingwa na wadau mbalimbali ikiwamo vyama vya siasa, imetajwa kuwa na uzito wa kipekee kiasi cha kuongezewa muda wa wiki moja tofauti na utaratibu wa kawaida wa bunge kukaa wiki mbili.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge imesema miswada ambayo imepangwa kujadiliwa katika mkutano huo ni Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023.
Miswada mingine ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 na muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023.
Vilevile katika mkutano huu wa Bunge Kamati za Kudumu za Bunge zitawasilisha taarifa za shughuli zlzotekelezwa na Kamati kwa mwaka 2023.
Aidha, taarifa hiyo imesema wastani wa maswali 250 ya kawaida na maswali 24 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yanatarajwa kuulizwa na wabunge.
Leave a comment