KAMPUNI ya Barrick Tanzania imenyakua tuzo sita katika kilele cha maadhimisho ya siku ya afya na usalama mahali pa kazi yanayofanyika katika Viwanja vya Tumbaku mjini Morogoro. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro… (endelea).
Katika maadhimisho hayo ambayo yanaratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa kazi (OSHA), Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu, umeshinda tuzo kubwa ya mshindi wa juu wa jumla katika Tuzo ya Afya na Usalama (OHS) 2023.
Mbali na ushindi huo mkubwa, Bulyanhulu pia ilinyakua tuzo ya uandaaji ripoti bora ya tathmini ya hatari katika uchimbaji madini na mshindi bora wa tuzo ya usalama na afya (OHS) katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Mgodi wa Barrick North Mara, ilishinda tuzo za juu katika: Kujali zaidi wafanyakazi wenye mahitaji maalum na utekelezaji sera bora ya usalama mahali pa kazi (OHS). Pia ilikuwa mshindi wa pili kwa washindi wa jumla wa sekta ya Madini.
Mwaka huu mgodi wa Buzwagi pia ulishiriki maonesho hayo na kunyakua tuzo ya utekelezaji mpango kazi bora wa usalama na afya mahali pa kazi.
Akizungumza katima kilele cha maadhimisho hayo Aprili 28, 2023 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Lazaro Ndalichako ambaye alikuwa mgeni rasmi alisisitiza waajiri kuzingatia sheria ya afya na usalama mahali pa kazi.
Aliwataka waajiri wote nchini kuchukua hatua ya kuhakikisha wanalinda usalama na afya za wafanyakazi wao kama yalivyomatakwa ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Namba 5 ya mwaka 2003.
Kampuni hiyo ya Barrick Tanzania imeshinda tuzo za 2023 kutokana na mafanikio ya 2022 ya kampuni ambapo ilishinda tuzo za jumla ikiwemo tuzo ya mshiriki wa maonyesho na tuzo ya kuzingatia kanuni za usalama.
Kampuni ina mpango maalum kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi wake na wakandarasi, kuhakikisha kwamba kila mtu anarudi nyumbani akiwa na afya njema na salama.
Leave a comment