March 2, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Babu Tale ashindwa kulipa deni, alala sero

Hamisi Taletale 'Babu Tale'

Spread the love

MENEJA wa msanii wa muziki wa Bongo fleva, Nasib Abdul ‘Diamond,’ Hamis Tale ‘Babu Tale’ amepelekwa rumande baada ya kushindwa kulipa fedha kama alivyoamuliwa na Mahakama Kuu. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Mahakama iliamuru Tale akamatwe baada ya kukiuka haki miliki ya kutumia masomo ya Mhadhiri wa dini ya kiislamu Sheikh Hashim Mbonde ambapo Mahakama ilimuamuru amlipe Mhadhiri huyo Sh. 250 milioni.

Mahakama ililiamuru jeshi la Polisi kumtia mbaroni Babu Tale Februari 16 mwaka huu na hakuweza kupatikana mpaka mahakama ikarejea wito huo tarehe 4 Aprili mwaka huu ambapo jana ndipo alipotiwa mbaroni.

Babu Tale amefikishwa mahakamani hapo leo saa 5:45 akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la Polisi ambapo Mahakama iliwapa muda yeye na mdeni wake kufanya mazungumzo ya suluhu nje ya Mahakama wakiafikiana watalipana walichokubaliana ambapo mazungumzo hayo yalishindwa kufikia muafaka.

Masajili wa Mahakama hiyo, Ruth Massam, ameeleza kuwa Jaji anayesikiliza kesi hiyo hayupo lakini kesi hiyo imeshindwa kutoa muafaka kutokana na Babu Tale kushindwa kulipa fedha taslimu kiasi cha Sh. 250 milioni.

Hivyo Babu Tale amerejeshwa mahabusu ya Polisi kituo kikuu cha Polisi cha kati (Central) mpaka muafaka wa kulipwa fedha kwa Sheikh Mbonde.

Sheikh Mbonde alikuwa akidai kuwa aliingia mkataba na kampuni ya kina Babu Tale ili wamrekodi mahubiri yake kisha wayauze na kugawana mapato.

Hata hivyo baada ya kurekodi masomo saba, walimkatia mawasiliano na alipowatafuta na kukutana nao wakamweleza kuwa wameamua kuachana na mpango huo.

Sheikh Mbonde alidai kuwa akiwa kwenye mahubiri Dodoma ndipo akakutana na mikanda ya video katika mfumo wa DVD yenye mahubiri yake huku kukiwa na namba za simu za viongozi hao wa Tip Top.

Sheikh Mbonde alidai baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa DVD hizo zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali, ndipo akawafungulia kesi ya madai ya fidia kutokana ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

error: Content is protected !!