VIJANA zaidi ya 30,000 wanatarajia kukutana tarehe 17 Disemba, 2022 kwa ajili ya kuliombea taifa wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadei Ruwa’ichi.
Askofu Thadei anatarajiwa kuongoza Ibada ya misa ya vijana hao katika mkesha wa kuliombea Taifa utakaofanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Akizungumzia mkesha huo, Katibu wa maandalizi wa mkesha huo, Ronaldo Chota alisema mkesha huo uliopewa jina la ‘Usiku wa sifa’, utafanyika usiku huo Jumamosi ambapo vijana watautumia katika kuliombea Taifa.
Chota aliongeza kuwa wanafanya hivyo kama ambavyo viongozi wa nchi wamekuwa wakihimiza watu kuliombea Taifa ambapo vijana wa vyuo zaidi ya 51 vikitarajiwa kushiriki.
Aliongeza kuwa sio mara ya kwanza kuwa na mkesha kwa ajili ya vijana kwani hata mwaka 2020 ulifanyika ambapo vijana 15,000 walihudhuria lakini kwa mwaka huu idadi hiyo itaongezeka na kufika hadi 30,000.
Hata hivyo, Mratibu huyo alieleza kuwa kwa vijana watakaofika katika mkutano huo pia watapata mafundisho yatakayowawezesha kupata hofu ya Mungu na kupata malezi bora ambayo yatakuja kuwasaidia kuwa viongozi bora wa kulitumikia taifa lao.
“Ni ukweli usiopingika kwa sasa kumekuwepo na changamoto nyingi zinazowakumba vijana ikiwemo mmomonyoko wa maadili unaopelekea kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo uasherati, kutoa mimba na mambo mengine hivyo mkesha huu utatumika katika kuyatafakari haya na kuona namna ya kuepukana nayo,” alisema Chota.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Walei Jimbo la Dar es Salaam, Padri Vitalisi Kasembo, aliwaomba wazazi kuwaruhusu vijana wao kuhudhuria mkesha huo utakaowasiadia kuwajenga kiimani.
Naye Mratibu wa Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Ludovic Kawishe, alisema usiku huo utasindikizwa na kwaya ya Mtakatifu Makuburi na Lord’s Grace Team na Mwalimu Arbogast Kanuti ndiye atakayehudumu.
Mkesha huo unatarajiwa kuanza saa tatu usiku mpaka saa 11 alfajiri.
Leave a comment