HALMASHAURI Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, imeiagiza Kamati ya Wasemaji ya Kisekta ya chama hicho kupaza sauti kuhusu changamoto ya kukithiri kwa tozo za Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, tarehe 5 Septemba 2022 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa ACT-Wazalendo, Janeth Rithe, akitoa maazimio ya kikao cha halmashauri hiyo kilichofanyika jana Jumapili, jijini Dar es Salaam.
Rithe amesema, mbali na kamati hiyo kupewa jukumu la kupaza sauti kuhusu tozo za Serikali, imetakiwa kujikita katika masuala ya uvunjifu wa haki za binadamu katika magereza na mageuzi katika Jeshi la Polisi, changamoto za bima ya afya na umuhimu wa hifadhi ya jamii.
“Halmashauri Kuu imeipongeza Kamati ya Wasemaji wa Kisekta kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuwasemea Watanzania. Aidha, Halmashauri Kuu imeagiza Kamati ya Wasemaji wa Kisekta kupaza sauti juu ya maeneo mahsusi ya kukithiri kwa tozo za Serikali, uvunjifu wa haki za binadamu magerezani, changamoto za bima ya afya na umuhimu wa hifadhi ya jamii na mageuzi katika Jeshi la Polisi,” amesema Rithe.
Katika hatua nyingine, Rithe amesema Halmashauri kuu hiyo imepitisha azimio la kuundwa kwa kitengo cha kusimamia uwajibikaji wa Serikali ya Zanzibar.
“Halmashauri Kuu imepitisha Azimio la kuundwa kwa Kitengo cha Chama cha Kusimamia Uwajibikaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Kitengo hicho kitakuwa na majukumu ya kufuatilia kwa karibu uwajibikaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kutoa sera mbadala,” amesema Rithe.
Leave a comment