Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kisa chopa, ziara ya Nape yaibua mjadala
Habari za SiasaTangulizi

Kisa chopa, ziara ya Nape yaibua mjadala

Spread the love

 

ZIARA ya Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye anayoifanya mikoa yote nchini kwa kutumia Helicopter ‘chopa’ kwa lengo la kukagua utekelezaji na kuhamasisha zoezi la anuani za makazi na postikodi, imeibua mjadala kuhusu gharama za ziara hiyo.

Nape ameanza ziara hiyo jana tarehe 11 kwa kutembelea mikoa Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hata hivyo, baada ya kutangaza ziara hiyo na kubainisha kuwa atatumia chopa, mjadala mkali umeibuka miongoni mwa wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa huku hoja kubwa ikielezwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma kutumia chombo hicho cha usafiri kukagua zoezi hilo.

Wachambuzi hao walienda mbali zaidi na kubainisha namna hali ya uchumi wa Taifa ilivyo tete katika kipindi hiki ambacho Serikali inahaha kupunguza makali ya mfumuko wa bei za bidhaa muhimu.

Pia walibainisha namna baadhi ya walimu zaidi ya 250 walioandamana mkoani Mwanza kudai posho zao baada ya kushiriki katika zoezi hilo la anuani za makazi na postikodi.

Mmoja wa wachangiaji katika mtandao wa Twitter, Heche Enock ambaye ameandika “Mh. @Nnauye_Nape naona una ziara ya kuzunguka nchi nzima kuhamasisha uwekaji wa anuani, hamna namna nyingine halmashauri zetu zinaweza kutumika kuhamasisha uwekaji wa anuani? Kwanini itumike gharama kubwa hivi? Kwanini mnatumia fedha za Umma vibaya kiasi hiki?

Hata hivyo, Nape alimjibu Enock na kumuonya kuacha kulaumu kabla ya kufanya uchambuzi.

“Gharama kubwa ni Tshs ngapi? Kabla kusema ni busara kuuliza! Tunapenda kulaumu bila kujipa muda kufanya uchambuzi. Unajua zinatumika Tshs ngapi ukilinganisha na tungezunguka kwa gari? Jipe muda halafu rudi kulaumu,” aliandika Nape.

Wakati Nape akitoa majibu hayo, mmoja wa wachambuzi kindakindaki wa siasa, Martin Maranja Masese kupitia ukurasa wake wa Facebook alimjibu Nape kwa kuchambua gharama hizo.

Masese alifafanua kuwa Helicopters aina ya H225 kwa wastani inatumia mafuta ya ndege (Jet-A1) galoni 540 kwa saa (kwa vipimo vya Marekani) ambapo kwa upande wa Tanzania ni sawa na lita 2,044.122 kwa saa.

Aliongeza kuwa gharama za kujaza katika Uwanja wa ndege Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) ni Dola za Marekani 3.612 au Sh 8,390.87 kwa galoni moja.

“Zingatia galoni moja kwa vipimo vya Marekani ni sawa na lita 3.785, hivyo kwa saa moja tu hiyo chopa hii inaweza kutumia wastani wa Shs. milioni 4.53 kwa safari ya saa moja angani kwa mafuta yake tu.

“Sijaweka gharama nyingine, maana lazima iruke ikiwa na operators wawili. Sifahamu kama operators wanalipwa na JWTZ au wizara, lakini zitakuwa fedha za umma.

“Naona taarifa hapa inaeleza ndugu Nape Nnauye atakwenda mikoa yote kuhamasisha uwekaji anuani za makazi (postikodi). Na leo (jana) Nape Nnauye ameanza kuruka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Shilingi ngapi zitatumika katika kurusha hii chopa ya JWTZ? Nani atagharamia hizo fedha? Alihoji Masese.

Aidha, Masese pia alihoji kuwa kwanini watendaji wa ngazi za chini wasiagizwe kusimamia zoezi la postikodi.

Alisema kuna wakuu wa mikoa, makatibu tawala mikoa, wakurugenzi wa majiji, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tarafa, watendaji wa kata na vijiji ambao walipaswa kufuatilia na kuhamasisha badala ya Waziri kutumia chopa.

“’Watasha’ wana msemo wao mzuri, wanasema “The bigger the helicopter, the larger its engine or engines and the more thirsty they become.”. Ndugu Nape ulipaswa kwanza kujiuliza hili swali “How much fuel does my bird burn per hour?”. Halafu ukipata jibu ndiyo uanze kuchoma fedha zetu.

“Helicopter ambayo inaweza kusafiri umbali mrefu kwa muda mrefu inahitaji mafuta mengi. Helicopters nyingi zina matenki yenye kubeba mafuta yatakoishi wastani wa saa 1.5 hadi saa 3 na dakika 20 za ziada. The Sikorsky S92 and the Agusta A139 zina matenki ya ziada. Pigeni hesabu,” aliongeza.

Alisema katika kipindi hiki cha mdororo wa uchumi na gharama za maisha kupanda, serikali ilipaswa kupunguza kuleta bajeti ya ziada kusaidia wananchi, kuondoa tozo kadhaa (hata kwa miezi sita tu) haswa katika bidhaa za mafuta yenye tozo 23 na serikali kupunguza matumizi yake ya anasa.

Aidha, hoja hizo ziliungwa mkono na kada maarufu wa CCM na mchambuzi wa masuala ya siasa, Thadeo Ole Mushi ambaye naye amepinga Nape kupitia andiko lake Facebook.

Mushi alisema kuna vitu vinakera sana wananchi na kuhoji iwapo kila waziri akirusha chopa kutembelea miradi itakuwaje?

“Waziri wa Elimu akahamasishe kuhusu ujenzi wa madarasa, wa Tamisemi akahamasishe ujenzi wa miundombinu, wa afya akahamasishe chanjo kwa chopa, wa mambo ya ndani arushe akahamasishe mambo ya NIDA gharama zitakuwaje?

“Vyombo vya habari havitoshi? katika karne ya sasa ambayo kupata habari ni kwa njia rahisi kabisa Waziri hawezi kuitumia kuhamasisha analotaka kulifanya?

Mushi alihoji sababu za Nape kuchagua usafiri wa chopa badala ya gari hasa ikizingatiwa zoezi ni la ukaguzi wa anuani za makazi.

“Wakati akitumia gharama kubwa namna hiyo wanaotumika kuifanya kazi hii huko Mwanza waliandamana hawajalipwa, na wengine wanalipwa fedha kidogo sana wakitumikia Taifa hili kwa uzalendo mkubwa, waziri yeye anataka kushinda hewani kama popo kwa gharama kubwa kiasi hicho.

“Bila kuhamasisha zoezi lilifikia asilimia 68 inahitaji nguvu kidogo sana tena kupitia kwa wakurugenzi ili kazi ikamilike kwa asilimia mia moja,” ameandika Mushi.

Mushi ameongeza kuwa Nape angechagua mikoa miwili au mitatu ambayo imefanya vibaya na kuitembelea ndipo atoe maagizo na kuongeza nguvu ili kazi ikamilike.

Aidha, kutokana na mijadala hiyo iliyobuka mitandaoni, leo Nape amerejea katika mtandao wa Twitter na kukoleza kuwa anafurahishwa na mijadala hiyo kuhusu ziara yake.

“Kwa heshima na unyenyekevu nafurahishwa/kufarijika na mjadala mkubwa na mzuri unaoendelea juu ya operesheni anwani za makazi. Mjadala huu ndio tulioutaka ili kulifanya zoezi hili liongeze kasi. Hakuna hoja tutaipuuza juu ya mjadala huu,zenye nia ya kujenga tutazifanyia kazi zote,” aliandika Nape.

2 Comments

  • Lol!
    Wazungu hawafanyi kazi namna hiyo. Wanatumia mnyororo wa amri na sheria. Pia, majibu yana rudi…hakuna kuzunguka zunguka. Mambo ya karne ya 20.
    Tungeanza na Mtwara au Sumbawanga.
    Je, ni sheria gani inasema anuani hizo zitumike?
    Kama mtu hataki kutumia itakuwaje?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RUWASA yachongewa, yateketeza mamilioni kwa maji yenye magadi

Spread the loveSAKATA la ukosefu wa maji wilayani Momba mkoani Songwe limezidi...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Lissu akabidhiwa gari lake, aomba msaada wa matengenezo

Spread the loveMakamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu leo Ijumaa amekabidhiwa...

error: Content is protected !!