Sunday , 19 May 2024
Home Kitengo Maisha Afya ACT-Wazalendo chalaani uzembe Serikali kusimamia utoaji huduma za afya
Afya

ACT-Wazalendo chalaani uzembe Serikali kusimamia utoaji huduma za afya

Spread the love

 

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelaani hatua “rahisirahisi” zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya mwenendo mbovu wa utoaji huduma za Afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Msemaji wa sekta ya Afya wa chama hicho, Dk. Nasra Omar, kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa jana Jumatano tarehe 6 Aprili, amesema chama kimefuatilia kauli na maagizo ya Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kuhusu mwenendo wa utoaji wa huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao hauridhishi na hauendani na maadili ya utumishi wa umma.

Itakumbukwa kuwa siku chache zilizopita Waziri Mollel alitoa miezi miwili ya hospitali hiyo kujitathmini uwezo wao wa usimamizi na utoaji huduma kwa wagonjwa.

“ACT Wazalendo inasikitishwa na hatua hizi ‘rahisirahisi’ zinazochukuliwa na Serikali linapokuja suala la uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hususani kwenye sekta ambayo imekabidhiwa hatima ya maisha ya wananchi wengi,” amesema Dk. Omar.

Amesema chama chao kimesikia vilio vya wananchi mijini na vijijini juu ya kutopata huduma sahihi na rafiki kwenye hospitali za umma na kuendelea kushuka kwa uwajibikaji kwa wahudumu wa sekta ya afya.

Hata hivyo amesema wanatambua uwepo wa changamoto ya kuelemewa kwa hospitali za umma kutokana na uwiano usiolingana wa wahudumu wa afya na wagonjwa wanaohitaji huduma.

“Uwiano wetu wa huduma za afya nchini uko kinyume na wastani wa viwango vya kimataifa (2017) ambapo Muhudumu mmoja wa afya anatakiwa kuhudumia wagonjwa 4000 kwa mwaka.
Amesema upungufu huo umetokana na serikali kutoajiri watumishi wa kutosha kwenye sekta ya afya ndani ya miaka sita iliyopita.

Aidha amesema, “zipo dalili za wazi za kushuka kwa hamasa ya utoaji wa huduma bora kwenye sekta ya afya, kuongezeka kwa kauli zisizoridhisha zinazotolewa kwa wagonjwa na kuporomoka kwa maadili ya wahudumu wa afya.”

Kutokana na hali hiyo amesema kauli iliyotolewa na Waziri haitibu changamoto zinazoikabili sekta ya afya hasa kwenye suala la uwajibikaji.

“Uwajibikaji wa wafanyakazi wa taasisi kubwa, nyeti kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni swala lisilohitaji msimu na matamko ya kisiasa,” amesema Dk. Omar.

Amesisitiza kuwa utoaji huduma rafiki kwa wagonjwa na kwa wakati ni wajibu wa watoa huduma na wataalam wa afya hususan kwenye hospitali za umma.

Amesema ili kuimarisha huduma ya afya na kuongeza uwajibikaji kwenye hospitali za umma, ACT-Wazalendo kinapendekeza Serikali kuongeza idadi ya wataalum wa afya kwenye hospitali za umma nchini ili kupunguza mzigo mzito kwa wahudumu, “hii moja kwa moja itadhibiti uzembe na kukosekana kwa uwajibikaji.”

Pia amesema Serikali iweke na kufuatilia utaratibu wa uwajibikaji kwa wahudumu wa afya katika hospitali zote za umma kuendana na kanuni, taratibu za utumishi wa umma, “hatuwezi kuendelea kuchukulia kwa urahisi kuporomoka kwa maadili, huduma bora kwenye sekta ya afya.”

Vilevile ameita Serikali iweke utaratibu na mfumo wa kielekroniki ambao ni rahisi kupokea malalamiko ya wananchi juu ya mienendo ya watumishi katika sekta ya afya na hali ya utoaji wa huduma.

Mbali na hayo ameitaka Serikali izijengee uwezo mamlaka na uongozi wa hospitali kuweza kujiendesha kupitia mfuko wa taifa wa afya.

“Lakini hili litawezekana endapo Serikali italipa madeni inayodaiwa hivi sasa kwenye mfuko wa taifa wa afya.”

ACT-Wazalendo pia kimeitaka Serikali kuimarisha huduma na usambazaji wa vifaa, vipimo na dawa katika vituo vya afya mijini na vijijini ili kupunguza msongamano wa wananchi wanaosubiri huduma kwenye hospitali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Afya

Kambi ya matibabu ya kibingwa Ruangwa yaacha vilio, DC atoa ombi JAI

Spread the loveMKUU wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma amefunga rasmi kambi...

AfyaHabari za Siasa

Serikali yatoa kauli wanaolala nje Hospitali ya Muhimbili

Spread the loveSERIKALI imesema inajipanga kushirikiana na sekta binafsi kujenga majengo yatakayosaidia...

Afya

Mbunge ataka huduma Ultrasound itolewe bure kwa wajawazito

Spread the loveMBUNGE wa Viti Maalum, Esther Malleko, ameitaka Serikali kutoa bure...

Afya

Vituo 13 vyasitishiwa mkataba madai kutaka kupiga bilioni 4 za NHIF

Spread the loveVITUO vya kutoa huduma za afya 13, vimesitishiwa mikataba ya...

error: Content is protected !!