Friday , 17 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mashahidi wakwamisha kesi ya Mbowe, yapigwa kalenda hadi Ijumaa
Habari za Siasa

Mashahidi wakwamisha kesi ya Mbowe, yapigwa kalenda hadi Ijumaa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, imeahirisha kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu hadi Ijumaa tarehe 4 Februari 2022, baada ya shahidi wa Jamhuri kupata dharura. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo iliyopangwa kusikilizwa mfululizo, imeahirishwa leo Jumanne, tarehe 1 Februari 2022 na Jaji Joachim Tiganga, baada ya kiongozi wa jopo la mawakili wa Jamhuri, Robert Kidando kuomba ahirisho la siku nbili (Jumatano na Alhamisi), kutokana na shahidi waliyepanga kumuita kupata dharura.

Wakili Kidando amedai, hawana shahidi mwingine kwa kuwa waliyetarajia kumuita ameshindwa kusafiri kutoka mkoani kuja Dar es Salaam, dharura ambayo iko nje ya uwezo wake ambapo alimuomba ahirisho ili wamtafute shahidi mwingine.

“Tunaomba ahirisho kuanzia tarehe 2 na 3 Februari, ndipo tutakapoweza leta shahidi mwingine sababu shahidi aliyejipanga aendelee baada ya shahidi huyu, mpaka jana alikuwa hajafika kutokana na dharura aliyotuambia iko nje ya uwezo wake,” amesema Kidando

Jaji Tiganga alikubali ombi hilo na kuagiza upande wa Jamhuri ulete shahidi siku ya Ijumaa bila kukosa, ili kesi hiyo iendelee kusikilizwa.

Wakili Kidando alitoa ombi hilo baada ya shahidi wa 12 wa Jamhuri, Askari wa Jeshi Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Denis Urio kumaliza kutoa ushahidi wake aliouanza Jumatano iliyopita.

Hata hivyo, Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Utetezi, Peter Kibatala alipinga ombi hilo akidai Jamhuri inaweza kuleta shahidi kesho kwa kuwa una mashahidi wengi ambao baadhi yao wanaishi Dar es Salaam.

“Sisi bila kuwakosea wenzetu hatujaona sababau ya msingi ya kuomba ahirisho yaani kwenye Committal (mwenendo wa mashtaka), mashahidi waliotajwa ni wengi,” amesema Kibatala na kuongeza:

“Tunashindwa kuelewa kwa nini tunaahirisha kesi sababu ya shahidi mmoja kati ya mashahidi kadhaa ambao hawajatoa ushahidi na kama tulivyosema mara kadhaa ni haki ya kikatiba wateja wetu kufahamu hatima yao mapema inavyowezekana.”

Hadi sasa upande wa Jamhuri umeita mashahidi 12 kati ya 24 iliyopanga kuita mahakamani hapo.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa JWTZ, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Udhibiti wa serikali wakera asasi za kiraia

Spread the loveBaadhi ya wadau wa demokrasia na viongozi wa asasi za...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Nape aomba bajeti ‘kiduchu’ kwa mwaka 2024/25

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Seneta: Wanasiasa hawasaidii mchakato wa Katiba mpya

Spread the loveSeneta wa jimbo la Busia, nchini Kenya, Okiya Okoiti Andrew...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

ACT-Wazalendo yasusia uchaguzi wa ubunge Zanzibar

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo, kimegoma kushiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo...

error: Content is protected !!