Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Kisa cha Panya, Kuku, Mbuzi na Ng’ombe
Habari Mchanganyiko

Kisa cha Panya, Kuku, Mbuzi na Ng’ombe

Spread the love

NYUMBANI kwa mwanadamu uliwekwa mtego wa panya, lengo likiwa kumnasa panya. Anaandika Babu Jongo … (endelea).

Panya alipoona mtego akamuambia kuku amsaidie kuutegua, kuku akakataa, akasema hakutegwa yeye kwa hiyo haumuhusu.

Panya akamfuata mbuzi, akamwambia amsaidie kuutegua, mbuzi akasema haumuhusu kwa kuwa hakutegwa yeye.

Panya hakukata tamaa, akamfuata ng’ombe akamuomba amsaidie kuutegua mtego, akiamini nguvu za ng’ombe hata kama akiukanyaga tu mtego utavunjika.

Ng’ombe akacheka kwa dharau akasema haumuhusu, akamjibu panya apambane na hali yake.

Siku moja usiku kwenye mtego aliotegwa panya akanasa nyoka, baba mwenye nyukba aliposikia kishindo kwenye mtego akajua panya tayari ameshanasa.

Baba akamtuma kijana wake akamuue panya aliyenasa kwenye mtego, kijana alipokwenda kichwakichwa akagongwa na nyoka, sababu mtegoni alinasa nyoka na sio panya.

Kijana akafariki baada ya kugongwa na nyoka. Asubuhi kulipokucha watu wakaanza kujaa msibani.

Kwa kuwa watu walikuwa wengi kiasi, usiku akachinjwa kuku ili kuwapa watu kitoweo.

Siku ya pili ya mazishi akachinjwa ng’ombe ili kukidhi haja ya kitoweo na siku ya tatu ya kuondoa tanga akachinjwa mbuzi.

Kumbuka mtego alitegwa panya, alipowaambia kuku, mbuzi na ng’ombe wamsaidie kuutegua kutokana na uwezo wao wakakataa sababu hawakutegwa wao.

Lakini sasa wote hao waliojiona hawahusiki wamechinjwa na panya bado yuko hai.

Wakati raia wa kawaida wanatekwa na kupotezwa kuna watu walisema “shauri yao sisi hayatuhusu.”

Wakati Ben Saanane alipotekwa wengine wakapaza sauti za kutaka haki za raia zizingatiwe, lakini wengine wakasema watajuana wenyewe na Chadema wenzao.

Aliposhambuliwa Tundu Lissu, wapo waliosema amezidi kusema hovyo, wacha yamkute.

Akapotezwa mwandishi Azory Gwanda, wengine wakasema watajuana na waandishi wenzao waliozidi kufukunyua yasiyowahusu.

Akatekwa Roma Mkatoliki, upande mmoja wakapiga kelele aachiwe akiwa hai wengine wakasema afe kabisa, eti nani alimtuma aimbe siasa za kukosoa.

Watu wakaendelea kutekwa hasa upande wasiounga mkono chama kilichopanga Ikulu, na wale wanaojiona wenye chama na nchi wakafurahia.

Akakamatwa Manji, mwenyekiti wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, akatupwa mahabusi, huyu ni mwanaccm kindakindaki, lakini baadhi ya mashabiki wa upande wa pili wakafurahia, wakatamani hata afilisiwe au afe kabisa, wengine bila kujali kuwa ni mwanaccm mwenzao.

Leo ametekwa Mohammed Dewj (MO), mwanaccm mwengine, mshirika wa karibu wa viongozi wengi serikalini na chamani.

Huyu ni mwanahisa kiongozi kwenye klabu ya Simba ya Dar es Salaam, ameshawahi kuwa mfadhili wa miaka mingi kwenye klabu hiyo.

Nuru inayowaka Simba kwa sasa inatokana na mkono wa MO, bahati mbaya tena yanatokea yaleyale.

Kuna mashabiki wa upande wa pili wanaomba MO asipatikane mpaka Ligi iishe au asipatikane kabisa akiwa hai.

Kutekwa kwa MO wao hakuwahusu, bado wanaamini wao wako salama.

Ni akili zilezile zilizotumiwa na kuku, mbuzi na ng’ombe, kuona mtego hawakutegewa wao.

Nani aliamini kama iko siku MO atatekwa kwenye ardhi ya Tanzania, tena asubuhi kweupe?

Nakuomba Mungu umsaidie MO apatikane akiwa hai na afya yake.

Lakini kipindi hiki ni muhimu kupata somo kwa wale waliokuwa wanajiona matukio haya hayatawagusa.

Ukiwa raia wa kawaida, mfuasi wa chama fulani, kiongozi wa chama, taasisi, serikali au hata dola – pinga, zuia upuuzi huu, jua nawe hauko salama hata kama unahusika na vitendo hivi vya utekaji.

BringBack MO Dewj & Others!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA wawanoa mama lishe 50 kukabiliana na majanga ya moto

Spread the loveKampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na...

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

error: Content is protected !!