SHIRIKA la kuwahudumia wakimbizi la Tanganyika (TCRS) lililopo mkoani hapa limewataka wafanyabiashara kutii sheria za miji na majiji zilizopo bila shuruti huku akiwaasa kufanya biashara kwa kujiwekea malengo na kuwa na nidhamu ya fedha. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).
Hayo yalisemwa jana na Msimamizi wa miradi wa Shirika la TCRS mkoa wa Morogoro, Rehema Samweli wakati akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara wadogo ulioandaliwa shirika hilo ukilenga kujadili hali halisi ya masoko kwa wafanyabiashara wadogo.
Rehema alisema, ni vema wakaacha tabia ya kufanya biashara kwa mazoea na kwa msemo wa bora siku ipite, bali wafanyeni biashara huku wakiwa wamejiwekea malengo madhubuti kwa ajili ya leo na kesho yao.
Alisema changamoto za wafanyabiashara ni nyingi na zinajulikana lakini aliwataka kwanza kutambua umuhimu wa kutii sheria ambazo zinawekwa na mamlaka lakini pia wawe na uvumilivu huku wote wakiwa na sauti moja yenye umoja.
Hata hivyo Rehema aliongeza kusema kuwa TCRS inatarajia kuanza kusaidia vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara wadogo wa mjini hapa kwa kuwaongezea mitaji ya biashara wanazozifanya katika vikundi vyao.
Alisema kuwasaidia kimikopo kutawafanya wafanyabiashara hao kuinuka na kuepokana na mlolongo mrefu wa masharti ya kupata mikopo na kutokopesheka kwa urais kutokana na kutokua na mali kubwa za ukopesheka kwenye vyombo vya kifedha kama dhamana.
Mmoja wa wafanyabiashara wadogo wa Manispaa ya Morogoro, Hassan Zuberi, alisema kuwa serikali na mashirika binafsi inapaswa kuwatazama wafanyabiashara wadogo kwa jicho la kuwainua kimaendeleo kwani ni kundi muhimu mno kwa maendeleo ya nchi.
Hata hivyo Zuberi alisema ni muhimu serikali ikaweka mikakati mizuri na kutoa mikopo kwa wingi na ikapunguza vigezo na masharti ya kupata mikopo ili vijana waweze kufanya biashara kwa tija huku wakikuza pato lao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia suala la ajira kwa vijana wanaotoa vyuoni Zuberi alisema Kila siku vijana wanamaliza vyuo vikuu na ngazi nyingine za elimu lakini suala la ajira za kuajiriwa wengi wao wanakosa na hujikita katika kufanya biashara ndogo ndogo ambapo alisema Serikali bado inahitaia kufanya kitu ili kuimarisha suala la ajira kwa vijana.
Leave a comment