Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge waliofukuzwa Chadema, watinga kwa Msajili
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge waliofukuzwa Chadema, watinga kwa Msajili

Spread the love

WABUNGE waliofukuzwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamekata rufaa ofisi ya msajili wa vyama vingi vya siasa kupinga uamuzi uliochukuliwa dhidi yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Wabunge hao ni;  Wilfred Lwakatare (Bukoma Mjini), Anthony Komu (Moshi Vijijini), David Silinde (Momba) na Joseph Selasini (Rombo).

Uamuzi huo wameuchukua ikiwa ni siku nne kupita tangu John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema kuutangazia umma maazimio ya kamati kuu ya chama hicho yaliyowavua uanachama.

Wabunge hao walifukuzwa wakituhumiwa kutotekeleza maagizo ya chama hicho ya kujiweka karantini kwa siku 14 ili kuangalia kama wana maambukizo ya corona au la.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa tarehe 1 Mei 2020 ndiye alitoa maagizo hayo ambayo hata hivyo, baadhi waliyapinga na kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge.

Leo Alhamisi tarehe 14 Mei 2020, MwanaHALISI Online limezungumza na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi kujua barua za rufaa za wabunge hao ambapo amesema, “Ni kweli barua tumezipokea na tunazifanyia kazi.”

Baada ya maelezo hayo ya Jaji Mutungi, MwanaHALISI Online limemtafuta Komu ambaye ni mmoja wa wabunge waliokata rufaa kujua kwa nini wamekwenda ofisini ya msajili na si kukata rufaa ndani ya chama ambapo amesema sheria inawaruhusu kufanya hivyo.

“Katika sheria,  kuna vifungu vinampa mamlaka msajili kuangalia mienendo ya chama na hata uamuzi uliofanywa na kama katiba na taratibu za vyama vimekiukwa,” amesema Komu

Amesema kuna njia tatu ambazo wangeweza kuzifanya ambazo mosi, ni kukata rufaa Baraza Kuu la Chama, “lakini tuliona tunaweza tusitendewe haki kutokana na miongoni waliohusika kutufukuza ni sehemu ya baraza hilo.”

Pili, ni kufungua kesi mahakamani, akisema, “unaweza kwenda mahakamani, lakini katiba yetu (ya Chadema) inasema ukienda mahakamani unakuwa umejifukuzisha chama ila pia, inachukua muda mrefu.”

Tatu, kwenda ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

“Sisi tumekwenda kwa msajili kwa sababu sheria imetupa hiyo fursa, kama ninyi waandishi wa habari mnaweza kwenda Baraza la Habari Tanzania (MCT) na sisi tumeamua kwenda kwa msajili,” amesema Komu ambaye amekwisha kusema mara baada ya Bunge kuvunjwa atahamia NCCR-Mageuzi

Akijibu swali, kwa nini wameamua kukata rufaa, Komu amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuona hawakutendewa haki ikiwamo kutoitwa na kuhojiwa juu ya tuhuma zilizokuwa zinawakabili.

“Utaratibu wa kutuchukulia hatua hazikufutwa. Tungeshtakiwa, tungejitetea na uamuzi usingekuwa huo waliouchukua,” amesema Komu

Katika maelezo yake, Komu amesema yeye ndiye aliyepeleka barua zote nne ofisi ya msajili jijini Dodoma ambapo, “nilipofika nikaenda masjala na kuwaeleza mmesoma vyombo vya habari, sisi tunapinga huo uamuzi (wa kutufukuza) na tunaomba hizi barua zifike mapema inavyowezekana.”

Komu amesema baada ya kuziwasilisha, aelezwa zitafikishwa kwa wahusika mapema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!